Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Stephen Chaya, ameishauri Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kutangaza mafanikio yaliyopatikana kupitia Kampeni ya Mama Samia Legal Aid ili wananchi na wadau waone matokeo ya utekelezaji wake.
Dkt Chaya ametoa ushauri huo alipotembelea Banda ya wizara hilo katika maonesho ya nane nane yanayoendelea katika Jijini Dar es salaam.
Dkt. Chaya ameipongeza Wizara hiyo kwa kuendelea kuwafikia wananchi kupitia huduma za msaada wa kisheria, akisema hatua hiyo imeleta mabadiliko makubwa kwa kusogeza huduma karibu na wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema ni muhimu mafanikio ya kampeni hiyo yaambatane na simulizi za wanufaika ili kuonesha matokeo halisi ya huduma zinazotolewa, jambo litakaloongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa msaada wa kisheria.

Aidha, amesema kampeni hiyo imewanufaisha wananchi wengi, hususan wa maeneo ya vijijini, ambao awali walishindwa kupata huduma za mawakili kutokana na gharama kubwa na umbali wa huduma hizo.
Dkt. Chaya amesema kupitia kampeni hiyo wananchi wamepata elimu ya sheria pamoja na msaada wa kisheria, hali iliyochangia kutatua migogoro mbalimbali na kuongeza uelewa wa haki na wajibu wao.
Ameongeza kuwa kuendelea kutangaza mafanikio ya kampeni hiyo kutasaidia kubaini maeneo yaliyofanikiwa na yale yenye changamoto, hivyo kuiwezesha Serikali kuweka mikakati bora zaidi ya kuboresha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Uzingatiaji wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Osboru Paissi amesema jumla ya wananchi 880 wamepatiwa huduma mbalimbali katika maonesho hayo ikiwemo kupatiwa elimu ya sheria, ushauri wa kisheria, uandaaji wa viapo, viapo vya kubadili majina na huduma nyingine za kisheria.
Amesema kuwa kati ya wananchi hao, 46 waliwasilisha migogoro kwa ajili ya kushughulikiwa, ambapo migogoro 11 tayari imetatuliwa na kufungwa, huku migogoro 35 iliyobaki ikiendelea kushughulikiwa katika hatua mbalimbali na mamlaka husika.

More Stories
Amana za Benki zinalindwa hadi Milioni 7.5
FAO yawataka wakulima kuzingatia kanuni bora za ufugaji
Wakulima waliowezeshwa na TADB waeleza mafanikio yao nanenane