Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline,Dodoma
SHIRIKA la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limewataka wakulima na wafugaji kuzingatia kanuni bora za ufugaji ili kupunguza usugu wa vimelea dhidi ya dawa (UVIDA) na badala yake wazingatie mbinu bora za ufugaji na matumizi sahihi ya dawa
Akizungumza leo Agosti 6,2026 katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mtaalamu wa Udhibiti wa Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa kutoka FAO, Dkt. Elibariki Mwakapeje, amesema matumizi holela ya dawa kwa mifugo na mazao yanachangia kuibuka kwa vimelea vinavyoshindwa kutibika kwa urahisi.
Amesema jambo hilo linaloongeza hatari ya maambukizi kwa binadamu na kuifanya tiba kuwa ngumu na ya gharama kubwa zaidi.
“FAO imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kuimarisha usalama wa chakula nchini, ikiwemo kufanya uchunguzi wa ubora wa maziwa katika maeneo ya wafugaji wa Kimasai na Simanjiro, ambapo matokeo yalionesha uwepo wa kiwango kikubwa cha vimelea”amesema
Amesema Shirika hilo limekuwa likitoa elimu kwa wafugaji kuhusu mbinu bora za ufugaji, usafi wa mazingira na uzalishaji wa maziwa salama ili kulinda afya ya walaji na kuongeza ubora wa bidhaa za mifugo.
Mwakapeje, amesema mafunzo hayo yamekuwa yakifanyika katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Ilala na Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Kihonda na Bigwa mkoani Morogoro, pamoja na Arusha, ambapo jumla ya wafugaji 185 walihitimu na kutunukiwa vyeti.
Amesema wahitimu hao wameendelea kuwa mabalozi wa elimu katika jamii zao, hatua iliyowezesha zaidi ya wafugaji 2,000 nchini kuanza kufuga kuku wa kisasa kwa kuzingatia mbinu bora zinazowapunguzia utegemezi wa matumizi ya dawa.

More Stories
Amana za Benki zinalindwa hadi Milioni 7.5
Dkt Chaya:Tagazeni mafanikio ya Kampeni ya mama Samia legal Aid
Wakulima waliowezeshwa na TADB waeleza mafanikio yao nanenane