August 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dar yajipanga kupokea washiriki 12000 Jukwaa la Africa50

Na Penina Malundo,Timesmajira

Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum 2026) yamekamilika, huku Tanzania ikiwa tayari kuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa utakaofanyika Agosti 5 hadi 6, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 4, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 12,000 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, wakiwemo Wakuu wa Nchi, viongozi wa taasisi za kifedha, wawekezaji, watunga sera na wadau wa maendeleo ya miundombinu.

Chalamila amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye atakayekuwa mwenyeji wa kuwapokea viongozi mbalimbali watakaoshiriki mkutano huo, unaolenga kuimarisha ushirikiano wa Afrika katika uwekezaji na maendeleo ya miundombinu.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye atakayekuwa mwenyeji wa kuwapokea viongozi wa mataifa mbalimbali watakaoshiriki mkutano huu muhimu kwa maendeleo ya Bara la Afrika,” amesema Chalamila.

Ameongeza kuwa miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kushiriki ni Marais wa Angola, Kenya, Msumbiji, Senegal na Nigeria, huku akibainisha kuwa jukwaa hilo litatoa nafasi ya kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya miundombinu, biashara na uwekezaji pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili Afrika.

Mbali na mijadala hiyo, washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzoefu, kujenga ushirikiano mpya wa kibiashara na kuainisha mikakati ya kuongeza mtaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yenye tija katika sekta ya miundombinu.

Kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania kunatarajiwa kuimarisha hadhi ya taifa kama kitovu cha mikutano ya kimataifa ya biashara na uwekezaji barani Afrika, sambamba na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi, uwekezaji na maendeleo endelevu ya miundombinu.