August 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Standard Chartered yatoa Mil 21.4 kuiwezesha CCBRT kuwajengea uwezo wanawake waliopona Fistula

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Benki ya Standard Chartered Tanzania kupitia Standard Chartered Foundation imetoa msaada wa Shilingi milioni 21.4 kwa Shirika la CCBRT ili kuimarisha programu ya Mabinti Program, inayowawezesha wanawake waliopona ugonjwa wa fistula kujitegemea kiuchumi baada ya kumaliza matibabu.

Msaada huo utatumika kununua mashine za kushona pamoja na kugharamia mafunzo ya kushona, kutarizi, ujasiriamali na usimamizi wa fedha kwa wanawake watakaonufaika na programu hiyo, kabla ya kukabidhiwa vitendea kazi vitakavyowasaidia kuanzisha shughuli za kujipatia kipato.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Standard Chartered Bank Tanzania, Jofrey Mchangila, amesema benki hiyo imeamua kuwekeza katika uwezeshaji wa wanawake kwa kuamini kuwa mwanamke anapoinuliwa kiuchumi hunufaisha familia na jamii kwa ujumla.

“Tumetoa mchango huu ili kusaidia wanawake waliopata matibabu ya fistula kujijenga upya kiuchumi. Watapatiwa mafunzo ya kushona, kutarizi, uendeshaji wa biashara na usimamizi wa fedha, kisha kila mmoja atapatiwa mashine ya kushona ili aanze kujitegemea,” amesema Mchangila.

Amesema huo si ushirikiano wa kwanza kati ya Standard Chartered na CCSBRT, kwani mwanzoni mwa mwaka huu, kupitia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, wafanyakazi wanawake wa benki hiyo walitoa mashine za kushona 12 pamoja na mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha kwa wanufaika wa programu hiyo.

Mchangila amesema uwezeshaji wa wanawake ni sehemu ya mkakati wa Standard Chartered Foundation wa kuchangia maendeleo ya jamii kupitia miradi yenye matokeo ya muda mrefu.

“Tunafahamu kwamba mwanamke anapowezeshwa kiuchumi, anaboresha maisha yake, familia yake na jamii inayomzunguka. Ndiyo sababu tunaamini programu hii inaendana kikamilifu na malengo yetu ya kuchangia maendeleo ya jamii,” amesema.

Ameongeza kuwa makabidhiano hayo yanafanyika wakati Standard Chartered duniani ikiadhimisha miaka 20 ya shughuli za kujitolea katika jamii, akisisitiza kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na CCSBRT ili kupanua wigo wa programu hiyo.Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT, Brenda Msangi, alisema shirika hilo linaendelea kutekeleza dhamira ya kuboresha maisha ya wananchi kwa kuunganisha huduma za afya na programu za uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake waliopona fistula.

Amesema Mabinti Program huwapatia wanawake hao mafunzo kwa kipindi cha miezi minne katika fani mbalimbali za kujiajiri, ikiwemo ushonaji na ujasiriamali, kabla ya kuwakabidhi vitendea kazi vinavyowawezesha kuanza biashara zao.

“Tunawapa wanawake hawa mafunzo ya ujasiriamali na stadi mbalimbali kwa miezi minne. Wanapohitimu wanapatiwa vitendea kazi, ikiwemo mashine za kushona, ili waanze kujipatia kipato na kusimama kwa nguvu kiuchumi,” amesema Msangi.

Amesema msaada wa Standard Chartered utaongeza uwezo wa programu hiyo kuwafikia wanawake wengi zaidi, akibainisha kuwa kila darasa hupokea wanawake 12 na tayari darasa la pili kwa mwaka huu linaendelea na mafunzo.Msangi alisema tangu CCBRT ianze kutoa huduma za matibabu ya fistula, imewahudumia zaidi ya wanawake 100,000, huku Mabinti Program ikiwa tayari imewawezesha takribani wanawake 200 kuanza maisha mapya baada ya matibabu.

“Kadri tunavyopata wadau wanaotushika mkono, ndivyo tunavyoongeza idadi ya wanawake tunaowafikia. Tunatoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kushirikiana nasi ili kuwajengea uwezo wanawake hawa na kuwasaidia kurejea katika familia na jamii wakiwa na maisha bora,” amesema.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza fursa kwa wanawake waliopona fistula kujitegemea kiuchumi, kurejesha matumaini yao na kuboresha ustawi wa familia pamoja na jamii kwa ujumla.