
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amewahimiza madereva wa bodaboda kujiepusha na makundi au vitendo vinavyoweza kuchochea uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa na ustawi wa shughuli za kiuchumi.
Itunda ametoa wito huo leo, Julai 29, 2026, aliposhiriki Mkutano Mkuu wa Madereva wa Bodaboda wa Jiji la Mbeya uliofanyika katika viwanja vya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Mbeya.
Amesema madereva wa bodaboda ni wadau muhimu wa maendeleo kwa kuwa hukutana na wananchi wengi kila siku, hivyo wanapaswa kuwa mabalozi wa amani na kushirikiana na Serikali katika kudumisha usalama wa jamii.
“Nyie ni watu muhimu sana katika jamii na mna wajibu wa kulinda amani yetu. Kundi hili lina mchango mkubwa kwa jamii inayotuzunguka. Nendeni mkawa mabalozi wazuri wa amani na uzalendo katika maeneo yenu,” amesema Itunda.
Aidha, amewataka madereva hao kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali, pamoja na kushiriki kikamilifu katika kulinda usalama wa wilaya kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola kuhusu vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha amani.
Kwa upande wao, madereva wa bodaboda wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani, kutoa taarifa za uhalifu kwa wakati na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuimarisha amani na utulivu katika Jiji la Mbeya.
Wamesema wanatambua nafasi yao muhimu katika jamii na kwamba wataendelea kuwa washirika wa Serikali katika kuhakikisha usalama barabarani unazingatiwa na amani inaendelea kudumishwa kwa manufaa ya wananchi wote.

More Stories
Chatanda sasa mlezi wa CCM Mara
Serikali kuzalisha Maelfu ya ajira kwa vijana kupitia sekta ya Umwagiliaji
Wanne wakamatwa kwa mauaji ya Mwalimu Dimoso