
Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline,Mbeya
JESHI la Polisi Wilaya ya Kipolisi Mbalizi limefanya matendo ya huruma kwa kuchangia damu na kushiriki katika zoezi la usafi katika Kituo cha Afya cha Mamlaka ya Mji Mdogo Mbalizi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono huduma za afya na ustawi wa jamii.
Shughuli hiyo iliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kipolisi Mbalizi (OCD), SSP Christopher Msonsa, akiwa ameambatana na maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Polisi.
Akizungumza baada ya shughuli hiyo leo Julai 28,2026, SSP Msonsa amesema Jeshi la Polisi linatambua kuwa ni sehemu ya jamii, hivyo lina wajibu wa kushiriki katika shughuli zinazochangia kuboresha afya za wananchi sambamba na kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda usalama wa watu na mali.
“Sisi ni sehemu ya jamii, hivyo tuna wajibu wa kushiriki katika shughuli zinazolenga kuboresha afya na ustawi wa wananchi. Kuchangia damu ni njia mojawapo ya kuokoa maisha ya watu wanaohitaji huduma hiyo,” amesema SSP Msonsa.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Mamlaka ya Mji Mdogo Mbalizi, Dkt. Maginya Mpuya, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kujitolea kuchangia damu na kushiriki katika zoezi la usafi, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza akiba ya damu salama kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.

Amesema damu iliyochangiwa itawanufaisha zaidi watoto, wajawazito, akina mama wanaopata changamoto wakati wa kujifungua na wagonjwa wengine wanaohitaji kuongezewa damu.
Dkt. Mpuya amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za umma na jamii katika kuboresha huduma za afya, huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kushiriki katika shughuli za kujitolea, ikiwemo uchangiaji wa damu, ili kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi.

More Stories
Mafuru akabidhiwa rasmi ofisi ya TANTRADE
Tanesco yatangaza katizo la umeme,kukamilisha mradi wa kilovoti 400
Tanzania yaeleza hatua za ushirikiano uhifadhi Ngorongoro