July 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mafuru akabidhiwa rasmi ofisi ya TANTRADE

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mkurugenzi Mkuu aliyemaliza muda wake wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Dkt. Latifa Khamis, amekabidhi rasmi ofisi kwa Mkurugenzi Mkuu mpya, Ephraim Balozi Mafuru, kufuatia uteuzi wake wa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano).

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TanTrade jijini Dar es Salaam, yakihudhuriwa na Menejimenti ikiwa ni ishara endelevu ya uongozi na utekelezaji wa majukumu ya mamlaka.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Dkt. Latifa amempongeza Mafuru kwa kuaminiwa kuiongoza TanTrade na kumtakia kila la heri katika kutekeleza majukumu yake ya kuendeleza na kukuza sekta ya Biashara, nchini.

Kwa upande wake, Mafuru amemshukuru Dkt. Latifa kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha TanTrade na kuahidi kushirikiana kwa karibu na Menejimenti, Wafanyakazi na wadau mbalimbali ili kuendeleza mafanikio yaliyopo, kukuza biashara ya ndani na nje ya nchi, na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.