July 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanasheria Mkuu afungua mkutano wa Mwaka wa TIArb

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari ameshiriki hafla ya Ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Mwaka wa Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TIArb) na Wiki ya Usuluhishi ya Dar es Salaam (DAR Arbitration week).

Hafla hiyo imefanyika Julai 22, 2026 Jijini Dar es salaam.Katika salamu zake kwa washiriki,Hamza Johari amewaeleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatambua umuhimu wa Usuluhishi katika kutatua migogoro ya Uwekezaji na Biashara kwa ujumla na kwamba suala hili ni chachu katika kuvutia uwekezaji na kukuza Uchumi wa Tanzania.

Aidha, amefafanua kuwa, azma ya Tanzania ni kuhakikisha Nchi inakuwa Kituo cha Usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji na biashara ya ndani na Nje ya Tanzania.

Amemalizia kuwa, katika mchakato wa kuhakikisha sheria za Tanzania zinaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Sheria ya Usuluhishi ni miongoni mwa Sheria ambazo zitarekebishwa ili kuhakikisha haziwi kikwazo katika kufikia Uchumi shindani na jumuishi kadri ya malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania,Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akimuwakilisha Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.