November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakiwa kufanya uchunguzi wa mifugo maabara inapougua

Na Dennis Gondwe,TimesMajira Olinbe,Dodoma

WANANCHI katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kufanya uchunguzi wa mifugo pindi inapougua kabla ya kuianzishia matibabu kutokana na uwepo wa maabara ya veterinari Kanda ya Kati.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Gratian Mwesiga alipokuwa akifungua kikao baina ya wataalam wa Mifugo na Wakala wa Maabara ya Veterinari Kanda ya Kati- Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Mwesiga alisema kuwa, kikao kazi baina ya Halmashauri ya Jiji na Wakala wa Veterinari Kanda ya Kati ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Jiji la Dodoma.

“Uwepo maabara hii ni jambo la manufaa katika utendaji kazi, kwa kuwa tupo katika Jiji ambalo ni makao makuu hivyo hatutakiwi kufanya kazi kwa kubahatisha. Hivyo, hata utekelezaji wa majukumu yetu lazima uendane na hadhi ya makao makuu. Niseme kuwa katika uchunguzi wa magonjwa, wataalam wetu hawatakuwa wakitibu mifugo kwa kubahatisha. Magonjwa yote yatakuwa yanachunguzwa kabla hayajaanza kutibiwa. Tulizoea kutibu kwa kutazama dalili za kwa sababu hatukuwa na namna ya kuchunguza,”alisema Mwesiga.

Mwesiga alitoa wito kwa wafugaji kutokubali mifugo yao kutibiwa bila kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara na kubaini tatizo. “Ugonjwa unaotibiwa lazima uchunguzwe kwanza na kufahamika, ndiyo matibabu yaanze,”aliongeza. Aidha, aliwataka maafisa mifugo katika ngazi ya Mitaa, Kata na Halmashauri kuacha tabia ya kutumia dawa ovyo kwa mifugo. Aliwataka kutumia huduma za Maabara ya Veterinari kutibu kulingana na aina ya ugonjwa.

Wakati huohuo, aliwataka wazalishaji wa vyakula vya mifugo na wafugaji kutumia fursa ya maabara hiyo kupima ubora wa vyakula vya mifugo. “Katika Halmashauri ya Jiji kumekuwa na malalamiko kwamba baadhi ya vyakula vya mifugo vipo chini ya kiwango. Wito wangu, waitumie maabara hii kupima ubora wa vyakula hivyo vinavyotumika katika mifugo ili tuwe na mifugo bora na mfugaji asipate hasara. Hili ni muhimu, unaweza kukuta mfugaji anajitahidi kutibu magonjwa yote, ila chakula kama ni kibovu, mifugo itaendelea kufa,”alisisitiza Mwesiga.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Kanda ya Kati- Dodoma,Dkt. Japhet Nkangaga alisema kuwa, kikao kazi hicho pamoja na mambo mengine kililenga kubainisha mbinu mbalimbali ambazo wakala yake inaweza kushirikiana na Jiji katika kudhibiti magonjwa ya wanyama katika Jiji la Dodoma.

“Tunatambua kabisa kuwa Jiji la Dodoma sasa hivi limepanuka baada ya kuwa Jiji rasmi na makao makuu ya nchi. Jiji limekuwa na muingiliano mkubwa wa wageni wengi, wanyama wengi, mifugo mingi inaingia. Hivyo, mahitaji ya wanyama, mahitaji ya mazao ya kutoka kwa wanyama na mahitaji ya nyama yameongezeka sana. Kwa hiyo, sisi kama wataalamu wa mifugo wajibu wetu ni kuangalia na kulinda afya za wanyama wetu ili kudhibiti magonjwa yoyote ambayo yanaweza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu,”alisema. Alisema kuwa, kama wakala hawawezi kufanya kazi peke yao bila kushirikiana na halmashauri katika kufikia mafanikio.

Alisema kuwa, wakala hiyo inashirikiana na halmashauri kwa sababu wana mamlaka ya kudhibiti na kusimamia kutokana na kuwa na watendaji katika ngazi ya kata na mitaa.

“Wito wangu kwa wananchi, kwanza washirikiane zaidi na wataalamu wa mifugo, wasitibu wala wasihisi kwamba kuona dalili fulani wakaamini kwamba ni ugonjwa fulani, wasiende kwa mazoea. Kwa hiyo, tunashauri watumie maabara zaidi kuchunguza mifugo yao ili wapate kubaini aina ya ugonjwa unaomsumbua mnyama ili uweze kutibiwa. Mnyama akitibiwa bila kufuata utaratibu, binadamu akaja kula ile nyama bado kunakuwa na yale mabaki ya dawa katika mwili wa mnyama. Binadamu anapokula matokeo yake, unakuta kunakua na magonjwa sugu hivyo, binadamu wanapata shida,”alisema Dkt.Nkangaga.

Aidha, aliongeza kuwa dhamira ya wakala yake ni kuhakikisha kuwa wananchi wa Jiji la Dodoma wanakuwa salama. Alisema kuwa, wanataka sekta ya mifugo na uvuvi iwe salama kwa ajili ya afya za binadamu.