July 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Milioni 750 kukamilisha kituo cha afya

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tanga,

SERIKALI imetoa ahadi ya kutoa kiasi cha sh.milioni 750 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyosalia kituo cha afya Maweni kilichopo jijini Tanga, hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo jirani.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha,Balozi Khamis Omar, alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Ambapo mbali na mradi  na kituo hicho  cha afya pia alikagua  mradi wa mabweni katika shule ya sekondari Usagara na kueleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Balozi Omar amesema,Serikali itaendelea kuelekeza fedha nyingi kwenye miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi hususani katika sekta za afya, elimu na miundombinu.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Mkoa wa Tanga umeendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miradi ya maendeleo, jambo linalodhihirisha dhamira ya kuboresha maisha ya wananchi.

“Kwa mwaka wa fedha uliopita, Mkoa wa Tanga ulipangiwa kutumia kiasi cha sh.bilioni 528.1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo,Serikali tayari imetoa kiasi cha sh.bilioni 487.5, sawa na zaidi ya asilimia 92 ya fedha zote zilizopangwa,”amesema Balozi Omar.

Katika hatua nyingine, Balozi Omar ameipongeza Bandari ya Tanga kwa usimamizi mzuri wa fedha za umma na mafanikio makubwa ya ukusanyaji wa mapato, akieleza kuwa uwekezaji uliofanywa na Serikali umeanza kuzaa matunda.

Amesema Serikali iliwekeza  kiasia cha sh.bilioni 429.1,kwa ajili ya  uboreshaji wa Bandari ya Tanga, huku bandari hiyo ikifanikiwa kukusanya mapato ya sh.bilioni 436, kiwango kilichozidi thamani ya uwekezaji huo na kusisitiza kuwa ni mfano wa matumizi sahihi ya fedha za umma.

Mganga Mkuu wa Jiji la Tanga, Dkt. Stephen Mwandambo,amesema kituo cha afya cha Maweni kitakapokamilika kitatoa huduma kwa zaidi ya wananchi  40,740 wa Kata ya Maweni ambao kwa miaka mingi walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, hususani za uzazi na matibabu ya dharura.

Amesema halmashauri hiyo  tayari imetenga  kiasi cha sh.milioni 75 katika mwaka wa fedha ujao kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya majengo muhimu yaliyobaki, ikiwemo kichomea taka, jengo la upasuaji na wodi ya wazazi.

Hata hivyo amesema ili kituo hicho kifikie hadhi ya kituo cha afya kamili  kinahitaji kujengwa majengo manane muhimu, yakiwemo jengo la utawala,mama na mtoto,wodi za wagonjwa, jengo la X-ray, nyumba za watumishi, jengo la kuhifadhia maiti, njia za kupitishia wagonjwa pamoja na uzio.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba,amesema  katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imetoa zaidi ya sh.bilioni 357 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jijini humo,kati ya fedha hizo sh.bilioni 1.8 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya sekta ya afya.

Ambapo hospitali ya Wilaya ya Masiwani ikipokea sh.bilioni 2.9 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma huku sh.milioni 548 zimetumika kujenga nyumba za watumishi na kuboresha vituo vya afya vya Mleni, Maweni, Pande na Chongoleani.

Kwa upande wake, mkazi wa Kata ya Maweni, Juma Abdala, amesema kukamilika kwa kituo hicho kutamaliza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa hivyo Serikali itekelezwe ahadi yake ya kutoa fedha za kukamilisha majengo yaliobakia.

Hata hivyo Mwenyekiti wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tanga, Meja Mstaafu Hamis Mkoba,ameiomba Serikali kusaidia kupatikana kwa kiasi cha sh.bilioni 24.7 za mapato ya kodi ambazo zimekwama katika baadhi ya taasisi tangu mwaka 2022.Huku  akisisitiza  kuwa fedha hizo zingechochea kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo jijini Tanga.

.