Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeibuka mshindi wa tatu katika kundi la Taasisi za Elimu ya Juu, Uwekezaji, Ujuzi na Utafiti kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), mafanikio yanayoakisi kuongezeka kwa imani ya wananchi katika elimu ya ufundi stadi, ubunifu na tafiti zinazotoa suluhisho kwa jamii.
Meneja wa Uhusiano wa VETA, Sitta Peter, amesema tuzo hiyo ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na taasisi hiyo katika kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi, ubunifu na teknolojia zinazochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza baada ya kufungwa kwa maonesho hayo, Sitta aliwashukuru Watanzania waliotembelea banda la VETA na kupata fursa ya kujionea huduma, bunifu na teknolojia mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.
Alisema banda la VETA lilitoa elimu kuhusu mafunzo ya ufundi stadi pamoja na kuonesha bunifu zilizotokana na tafiti zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili jamii na sekta za uzalishaji.
Sitta alieleza kuwa VETA inaendelea kufanya tafiti zinazozalisha ubunifu unaojibu mahitaji halisi ya wananchi na kusaidia kuongeza tija katika uzalishaji na maendeleo ya uchumi.
Aidha, alisema elimu ya ufundi stadi ina mchango mkubwa katika kupunguza ukosefu wa ajira kwa kuwawezesha wahitimu kujiajiri, kuanzisha biashara na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.
Aliongeza kuwa ushindi huo ni chachu kwa VETA kuendelea kuboresha mafunzo, ubunifu na huduma zake ili kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kukuza uchumi wa Taifa.
“Biashara nyingi haziwezi kukua bila kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi. Ndiyo maana VETA itaendelea kusisitiza mafunzo ya ufundi stadi na ujasiriamali ili wahitimu wetu waweze kujiajiri na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi,” amesema Sitta.

More Stories
PPRA yashinda Tuzo, yaahidi kuendelea kuhudumia wananchi
Dkt.Mwinyi awahimiza Wafanyabiashara kutumia fursa za Masoko
Kapinga amwezesha mwenye ulemavu Mashine kusaga viungo