July 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Latifa:Sabasaba yafungua milango ya masoko ya Kimataifa

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Katika mafanikio yanayoonesha kuongezeka kwa ushawishi wa Tanzania katika biashara za kimataifa, Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamewezesha mauzo ya papo kwa papo kufikia Shilingi bilioni 3.9 na kuzalisha maombi ya awali ya kuuza bidhaa nje ya nchi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.1.

Akizungumza wakati wa kufungwa kwa maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Dkt. Latifa Khamis, amesema takwimu za awali zinaonesha kuwa Sabasaba imeendelea kuwa daraja muhimu la kuwaunganisha wazalishaji wa ndani na wanunuzi wa kimataifa, huku ikifungua fursa mpya za masoko kwa bidhaa za Tanzania.

Amesema utafiti uliofanywa kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebaini kuwa zaidi ya asilimia 91 ya waoneshaji walipata wanunuzi au washirika wapya wa biashara, jambo lililochochea ukuaji wa biashara na uwekezaji.

Kwa upande mwingine, ushiriki wa Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC) umeendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya China na Afrika Mashariki. Kampuni hiyo imesema zaidi ya wazalishaji 700 kutoka China wameshiriki katika maonesho ya Sabasaba tangu mwaka 2021, hatua iliyochangia kuongezeka kwa mikataba ya biashara na uwekezaji kati ya pande hizo mbili.

Mwakilishi wa EACLC, Lissa Wang, amesema Tanzania na Zanzibar zina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha biashara na usambazaji wa bidhaa katika Afrika Mashariki na ukanda wa SADC kupitia uwekezaji unaoendelea katika miundombinu ya biashara na usafirishaji.

Amesema kampuni hiyo inaendelea na ujenzi wa ghala la forodha na kituo cha usambazaji wa bidhaa Zanzibar, mradi unaolenga kuimarisha biashara ya mipakani na kuongeza mtiririko wa bidhaa katika ukanda huo.

Mafanikio hayo yanaifanya Sabasaba kuendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, huku likichochea ukuaji wa biashara, uwekezaji na upatikanaji wa masoko mapya kwa bidhaa za Tanzania.