Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
AFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Nicodemus Mkama, amesema kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Kampuni ya iTrust Finance Limited maarufu kama iTrust Bond katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ni hatua kubwa katika maendeleo ya masoko ya mitaji nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Kampuni ya iTrust Finance Limited, yaani iTrust Bond, katika Soko la Hisa la Dar es Salaam leo , CPA. Mkama amesema hatifungani hiyo imeweka historia kwa kuvunja rekodi kadhaa katika sekta ya masoko ya mitaji.
Amesema rekodi ya kwanza ni kuwa iTrust Bond imekuwa hatifungani ya kwanza kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam iliyotolewa na kampuni yenye Leseni ya Uwakala wa Soko la Hisa (Licensed Broker/Dealer) pamoja na Leseni ya Usimamizi wa Mifuko ya Uwekezaji (Fund Manager) iliyotolewa na CMSA.
“Pili, ni hatifungani ambayo mauzo ya toleo la kwanza yameweza kuzidi kiasi cha programu nzima ya hatifungani yenye thamani ya sh. bilioni 100 iliyokuwa itolewe katika awamu nne ndani ya miaka minne,” amesema CPA. Mkama.
Ameeleza kuwa programu hiyo ilikuwa inalenga kutoa shilingi bilioni 15 mwaka 2026, bilioni 20 mwaka 2027, bilioni 30 mwaka 2028 na bilioni 35 mwaka 2029, lakini mafanikio yaliyopatikana yamevuka matarajio hayo.
CPA. Mkama amesema mauzo ya iTrust Bond yamepata mafanikio ya asilimia 760.78 baada ya kupatikana kwa shilingi bilioni 114.12, ikilinganishwa na shilingi bilioni 15 zilizotarajiwa.
“Mafanikio haya yameifanya Hatifungani ya iTrust kuweka historia ya kuwa hatifungani iliyopata mafanikio makubwa zaidi kuliko zote zilizowahi kutolewa hapa nchini. Rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Hatifungani ya MAKAZI Bond ya kampuni ya First Housing Finance Limited yenye mafanikio ya asilimia 661.1,” amesema.
Ameipongeza iTrust Finance Limited kwa kuvunja rekodi hiyo na kuendelea kuwa mfano wa matumizi bora ya fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji kwa ajili ya kukuza biashara na kuchangia maendeleo ya uchumi.
Kwa mujibu wa CPA. Mkama, tangu mwaka 2021 wakati kampuni hiyo ikijulikana kama Imaan Finance Limited hadi sasa ikiwa iTrust Finance Limited, imeendelea kutumia fursa za masoko ya mitaji kupitia utoaji wa Hatifungani, Sukuk na Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.
Amesema juhudi hizo zinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanayolenga kuona sekta ya fedha ikiwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kukuza sekta binafsi, sekta ya umma na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Aidha, amebainisha kuwa kati ya wawekezaji waliowekeza katika iTrust Bond, asilimia 66.66 ni wawekezaji mmoja mmoja (Retail Investors) huku asilimia 33.34 wakiwa ni kampuni na taasisi (Institutional Investors).
Ameongeza kuwa asilimia 98.82 ya wawekezaji ni wa ndani ya nchi, huku asilimia 1.18 wakiwa wawekezaji wa kigeni, hali ambayo amesema inaonesha kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika masoko rasmi ya fedha.
CPA. Mkama amesema kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo kumeongeza thamani ya uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni na Taasisi kwa asilimia 5.46 na kufikia shilingi trilioni 2.20 kutoka shilingi trilioni 2.09.
Aidha, amesema amefurahishwa na matumizi ya teknolojia katika mchakato wa uwekezaji ambapo takribani asilimia 89 ya maombi yote yalifanyika kupitia mifumo ya kidijitali, huku mfumo wa iTrust App ukichangia zaidi ya asilimia 71 ya maombi yote.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana pia na mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayotolewa na Serikali katika kukuza masoko ya mitaji, ikiwemo kuondolewa kwa kodi ya zuio (withholding tax) kwenye faida za hatifungani za kampuni na taasisi.
Pia amesema CMSA iliruhusu kupunguzwa kwa kiwango cha chini cha uwekezaji katika iTrust Bond kutoka shilingi milioni moja hadi laki tano, hatua iliyoongeza ushiriki wa wawekezaji wengi hususan vijana na wanawake.
Ameongeza kuwa ubunifu wa kulipa riba ya hatifungani hiyo mara nne kwa mwaka badala ya mara mbili umeongeza mvuto kwa wawekezaji kwa kuwawezesha kupata ukwasi na kipato kwa muda mfupi.
Katika hatua nyingine, CPA. Mkama amezitaka kampuni na taasisi za sekta binafsi na umma kutumia fursa za masoko ya mitaji kupata fedha za kukuza biashara na kugharamia miradi ya maendeleo.
Amesema CMSA itaendelea kusimamia mikakati yenye lengo la kuchochea maendeleo ya masoko ya mitaji na kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Kitengo cha ushauri na Utafiti wa iTrust Bond Samali Shirima alisema fedha zilizopatikana kupitia hatifungani hiyo zitatumika kuimarisha mifumo ya kidijitali ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuwafikia Watanzania wengi zaidi.
Aliongeza kuwa matumizi ya masoko ya mitaji yanaendelea kuwa njia muhimu kwa taasisi na kampuni kupata mtaji wa kuendeleza shughuli zao, huku yakichangia pia ukuaji wa uchumi na ongezeko la mapato ya Serikali kupitia kodi.




More Stories
Waziri Mkuu mgeni rasmi uzinduzi wa kitabu cha “Mama Samia Doctrine of Law”
Serikali yaahidi kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI
TARI Selian yawaalika wakulima maonesho ya Kilimo-biashara