Na Joyce Kasi
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Dkt. Evelyn Munisi, leo ametembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo amejionea huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi na kutoa maelekezo ya kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kuhusu masuala ya kazi, ajira na usalama mahali pa kazi.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Dkt. Evelyn amesema ameridhishwa na namna wananchi wanavyopata elimu kuhusu haki na wajibu wao katika maeneo ya kazi, ikiwemo masuala ya usalama na afya kazini, pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria za kazi kwa waajiri na wafanyakazi.
Amesema banda hilo limekuwa fursa muhimu ya kusikiliza na kutatua changamoto pamoja na kupokea maoni na malalamiko ya wananchi kuhusu masuala ya kazi na ajira, huku wataalamu wakitoa ushauri na ufafanuzi wa sheria na taratibu mbalimbali za Serikali. Aidha, Dkt. Evelyn ameeleza kufurahishwa na elimu inayotolewa kwa vijana, hususan wanawake, kuhusu fursa za kuongeza ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la sasa linaloendeshwa na maendeleo ya teknolojia na ubunifu.
“Leo dunia inahitaji watu wenye ujuzi na uwezo wa kutumia teknolojia. Serikali tayari imeanza kutekeleza programu mbalimbali za kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya stadi na ujuzi ili waweze kujiajiri na kuajiriwa kwa ushindani,” amesema Dkt. Munisi
Ameongeza kuwa katika siku za hivi karibuni ametembelea baadhi ya vituo vya mafunzo ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa programu hizo na kubaini kuwa hatua zinazochukuliwa zinaendelea kuleta matokeo chanya. Dkt. Evelyn amewahakikishia Watanzania kuwa, kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali katika maendeleo ya ujuzi na teknolojia, katika miaka michache ijayo nchi itakuwa na wataalamu wa kutosha katika sekta mbalimbali.
“Ninawaambia Watanzania kuwa katika miaka michache ijayo hatutakuwa na utegemezi mkubwa wa wataalamu kutoka nje ya nchi. Tutakuwa na wataalamu wetu wenye uwezo wa kutoa huduma na hata kufundisha wengine. Haya ndiyo maelekezo na dira ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya Taiga,” amesisitiza.

More Stories
Mahundi afichua nguzo Muhimu kwa familia imara
Polisi Mbeya yakamata wanachuo wanne kuhamasisha vurugu
WMA yazidi kuwafikishia elimu Wajasiriamali