Na.Penina.Malundo,Timesmajira
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania Devid Misime amesema hali ya usalama nchini inaendelea kuwa shwari kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya wananchi, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau mbalimbali.
Ameyasema Leo kwenye maonesho ya 50 ya Sabasaba,Misime amesema licha ya hali ya utulivu uliopo, Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kufuatilia kwa karibu viashiria vya baadhi ya watu wachache wanaodaiwa kupanga kuvuruga amani kwa kutumia visingizio vya kufanya maandamano yasiyofuata taratibu za kisheria na kiusalama. Amesema baadhi ya watu hao tayari wamekamatwa huku uchunguzi ukiendelea ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Ameeleza kuwa uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya watu wanaendelea kuhamasisha vurugu kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya majadiliano, wakidaiwa kupanga kufanya vitendo vya uhalifu ikiwemo kushambulia viongozi na wananchi, kuchoma shule, kuharibu na kupora mali za umma na binafsi pamoja na kuwashambulia askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kupora silaha.
Msemaji huyo amesema uhamasishaji wa aina hiyo ni tishio kwa usalama wa taifa na ni kinyume cha sheria, hivyo Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa mtu au kikundi chochote kitakachojihusisha na vitendo hivyo, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya uhalifu pamoja na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarisha ulinzi nchini kote, hususan kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Sabasaba na Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba, ili kuhakikisha wananchi wanashiriki na kurejea majumbani salama.
Msemaji huyo amewahakikishia wananchi kuwa wasiwe na hofu bali waendelee na shughuli zao za kila siku kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara na vinaendelea kushirikiana kuhakikisha amani, utulivu na usalama vinaendelea kudumishwa nchini.
Pia ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi au vyombo vingine vya ulinzi na usalama endapo watabaini viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani au ukiukwaji wa sheria, ili hatua za haraka na stahiki ziweze kuchukuliwa.

More Stories
Vodacom yang’ara sabasaba,yatwaa tuzo mbili
TTB yamteua khalid al barwani kuwa Balozi wa Utalii
Serikali yaongeza kasi Mpango wa Umeme Nyuklia