Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
Kampuni ya GF Trucks and Equipment imeeleza kufurahishwa na mafanikio yake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), baada ya kutwaa tuzo ya banda bora kwa mwaka wa pili mfululizo huku ikiahidi kuendelea kuleta teknolojia bunifu na rafiki kwa mazingira nchini.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mwakilishi wa kampuni hiyo, Salman Karmali, amesema mafanikio hayo ni ishara ya imani ambayo kampuni imejijengea kwa wadau na wananchi kupitia ushiriki wake wa muda mrefu katika maonesho hayo.
Amesema GF Trucks and Equipment imekuwa mshiriki wa maonesho ya Sabasaba kwa miaka mingi na imeendelea kutumia jukwaa hilo kuwatambulisha Watanzania bidhaa na teknolojia mpya zinazolenga kuongeza ufanisi katika sekta mbalimbali za uchumi.
Karmali amesema maonesho ya mwaka huu, yanayoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, yamevutia idadi kubwa ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na kampeni kubwa ya uhamasishaji iliyofanywa na waandaaji.
“Ni heshima kubwa kwetu kupata tuzo hii kwa mwaka wa pili mfululizo. Tunawashukuru viongozi wa TanTrade kwa kutupa heshima hii na kutuongezea hamasa ya kuendelea kuboresha huduma na bidhaa zetu,” amesema.

Amebainisha kuwa katika maonesho ya mwaka huu kampuni imewasilisha bidhaa mbalimbali zikiwemo magari madogo, malori, mitambo mizito pamoja na mashine za kisasa za utafiti na uchimbaji maji.
Kwa mujibu wake, moja ya vivutio vikubwa katika banda lao ni mitambo ya dozer pamoja na mashine za utafiti na uchimbaji zinazojulikana kama drilling rigs au exploration rigs, ambazo hutumika katika tafiti za vyanzo vya maji na shughuli nyingine za uchimbaji.

Amesema baadhi ya mitambo hiyo imebuniwa kwa kuzingatia mazingira na mahitaji ya Tanzania baada ya kufanyiwa tafiti za kina ili kuhakikisha inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Karmali amesema kampuni hiyo inaendelea kuunga mkono juhudi za kuhifadhi mazingira kwa kuleta teknolojia zinazopunguza matumizi ya mafuta na kupunguza athari kwa mazingira.
“Kwa sasa dunia inaelekea kwenye matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira. Sisi tumekuja na bidhaa zenye matumizi madogo ya mafuta na pia tumewaletea magari yanayotumia umeme ya chapa ya Hyundai, ambayo tayari yameanza kutambulishwa nchini,”amesema.

Ameongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea kutoa ofa maalum kwa wateja wake hadi mwisho wa maonesho hayo na kuwahimiza wananchi pamoja na wadau wa sekta mbalimbali kutembelea banda lao ili kujionea teknolojia mpya zinazowasilishwa na kampuni hiyo.
Mwaka huu wa maadhimisho ya miaka 50 ya Sabasaba, GF Trucks and Equipment imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuleta suluhisho za kisasa katika sekta ya usafirishaji, ujenzi na uchimbaji, huku ikijikita katika matumizi ya teknolojia endelevu na rafiki kwa mazingira.

More Stories
Dkt.Samia aitangaza Sabasaba kama nguzo ya Biashara,Uwekezaji
Wizara yahamasisha Watoto kuhusu Nishati Safi
Balozi Omar akoshwa na usimamizi Matumizi ya Moduli