Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
CHAMA cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu Tanzania (CHAKUHAWATA) kimeiomba Serikali kupitia Waziri Mkuu kuelekeza Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha maafisa utumishi na waajiri katika halmashauri zote nchini wanafuata sheria na kuacha kuwazuia walimu wanaotaka kujiunga na chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Julai 3, 2026, Mwenyekiti wa Taifa wa CHAKUHAWATA, Emanuel Herman,amesema bado kuna baadhi ya wilaya ambako walimu wanaowasilisha maombi ya kujiunga na chama hicho hukumbana na vikwazo kutoka kwa waajiri, jambo alilosema linakiuka haki ya mfanyakazi ya kuchagua chama anachotaka kujiunga nacho.

Herman amesema pamoja na kuwepo kwa Waraka Na. 1 wa Katibu Mkuu, Utumishi wa Umma wa mwaka 2013, ambao unawaelekeza waajiri kutekeleza maelekezo ya mfanyakazi kuhusu makato ya ada za uanachama na kuruhusu mfanyakazi kujitoa katika chama cha awali na kujiunga na chama kingine anachokichagua kwa hiari yake, bado baadhi ya maafisa utumishi hawaelekezi makato kwenye chama alichokichagua mwalimu.
Amesema hali hiyo husababisha walimu kuendelea kukatwa ada za chama wasichokitaka, kinyume na matakwa ya sheria na taratibu za utumishi wa umma.
Alibainisha kuwa Mkutano Mkuu wa Taifa unaofanyika kwa sasa unalenga kufanya marekebisho ya rasimu ya Katiba ya CHAKUHAWATA kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Msajili baada ya rasimu hiyo kuwasilishwa kwa ajili ya usajili.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wanawake wa CHAKUHAWATA Prisca Cheyo kutoka Urambo amesema chama kimejipanga kukamilisha marekebisho yote yaliyoelekezwa ili katiba hiyo ipitishwe na kukidhi matakwa ya kisheria.

Amesema chama kinaendelea kukua na kupata wanachama wengi, huku changamoto za awali zilizotokana na kutotambulika kwake zikizidi kupungua baada ya walimu na waajiri kuelewa kuwa lengo lake ni kulinda na kutetea maslahi ya walimu.
Herman pia alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kile alichokiita ushirikiano na mazingira mazuri yanayowezesha walimu kutumia haki zao za kikatiba, akisema viongozi mbalimbali wa serikali mikoani wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa chama hicho.
Amesema licha ya mafanikio hayo, bado kuna baadhi ya Halmashauri ambako walimu wanaowasilisha fomu za kujitoa katika vyama vya awali na kujiunga na CHAKUHAWATA hukwamishwa na waajiri, jambo linalosababisha malalamiko kutoka kwa wanachama.
Naye Katibu wa CHAKUHAWATA Wilaya ya Karagwe, Helbinus Cyprian,amesema chama kina mshikamano mkubwa kati ya viongozi na wanachama wake, lakini changamoto ya baadhi ya waajiri kutotekeleza maelekezo ya walimu kuhusu uanachama bado ipo katika maeneo mbalimbali.
Alikumbusha kuwa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004, kifungu cha 9, inampa mfanyakazi haki ya kuunda au kujiunga na chama cha wafanyakazi anachokichagua bila kulazimishwa, na kuitaka Serikali kuhakikisha sheria hiyo pamoja na waraka wa Katibu Mkuu wa Utumishi vinatekelezwa ipasavyo ili kulinda haki za walimu nchini.


More Stories
DCEA yawanoa waandishi wa habari kuhusu kemikali bashirifu
SCADA yaimarisha ufanisi katika Shughuli zake
Wananchi wawezeshwa kutambua dawa za kulevya Sabasaba