Na Joyce Kasiki


BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limewahimiza wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kupata taarifa sahihi kuhusu elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, pamoja na kushuhudia mafanikio ya mkondo wa elimu ya amali unaotekelezwa katika shule za sekondari.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa NACTVET, Dora Tesha, amesema maonesho hayo ni fursa muhimu kwa Baraza kuwafikia wananchi na wadau mbalimbali kwa lengo la kuwapa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
Amesema kupitia banda la NACTVET, wananchi wanapata taarifa kuhusu vyuo vinavyosimamiwa na Baraza, programu za masomo zilizoidhinishwa, taratibu za kuomba nafasi za masomo, pamoja na hatua za usajili wa vyuo vipya vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
“Vilevile tunatoa huduma kwa wahitaji wa vyeti vya matokeo ya masomo na kuwapatia mwongozo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na NACTVET. Tunawahimiza wananchi kufika katika banda letu ili wapate taarifa sahihi na huduma kwa wakati,” amesema Tesha.
Aidha, amesema kivutio kikubwa katika maonesho ya mwaka huu ni ushiriki wa wanafunzi wanaosoma mkondo wa elimu ya amali katika shule za sekondari, ambao wanaonesha kwa vitendo ujuzi walioupata kupitia mfumo huo mpya wa elimu.
Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa mkondo wa elimu ya amali kumetokana na maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, yenye lengo la kuwajengea vijana ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa mara baada ya kuhitimu masomo.
“Tunawakaribisha wananchi kutembelea banda letu ili wajifunze kuhusu huduma za NACTVET, lakini pia wajionee matokeo ya uwekezaji wa Serikali katika kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira,” amesema.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bwiru Boys, Daudi Elias, anayesoma kidato cha tatu, amesema kujiunga na mkondo wa elimu ya amali kumemsaidia kupata mwelekeo wa maisha na kumjengea uwezo wa kujitegemea kupitia ujuzi anaoupata.
Amesema tofauti na ilivyokuwa awali, sasa wanafunzi wana nafasi ya kupata ujuzi unaowawezesha kuanza kujitegemea hata kabla ya kuendelea na masomo ya juu.
Daudi ameshauri Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kuongeza walimu wa masomo ya amali pamoja na vitabu na vifaa vya kufundishia, ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike na mfumo huo wa elimu unaozingatia ujuzi na ubunifu.:
Kwa upande wake, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Baobab jijini Dar es Salaam , Caren Mark, anayesoma mkondo wa Elimu ya Amali katika fani ya Electrical Installation, amesema amechaguliwa na NACTVET kushiriki maonesho hayo ili kuwakilisha shule yake na wanafunzi wanaosomea umeme.
Amesema ushiriki wake unalenga kuonesha ujuzi alioupata darasani na kutoa hamasa kwa wasichana kujitokeza kusomea fani za ufundi ambazo kwa muda mrefu zimeonekana kuwa za wavulana pekee.
Caren amesema katika banda la NACTVET anaonesha mradi wa vifaa vya umeme vya majumbani unaojumuisha mfumo wa usalama unaotumia kengele, taa zinazowashwa na mfumo wa sensor pindi kunapokuwa na giza, pamoja na teknolojia zinazoweza kutumika katika nyumba, shule, hospitali na maeneo mengine
. Amesema elimu ya amali imemjengea uwezo wa kubuni na kutengeneza mifumo hiyo, huku akiwahimiza wanafunzi, hususan wasichana, kujiamini na kuchagua masomo ya ufundi kwa kuwa yanatoa fursa kubwa za ajira na kujiajiri.

More Stories
Wananchi wawezeshwa kutambua dawa za kulevya Sabasaba
Balozi Omar akoshwa na usimamizi matumizi ya Moduli
GASCO yaeleza majukumu sabasaba, yaboresha miundombinu Gesi