Na Mwandishi wetu
TAASISI ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imewakumbusha wakulima na wadau wa sekta ya kilimo kununua mbegu zilizofungashwa na zenye taarifa zote muhimu, ikisisitiza kuwa sheria hairuhusu uuzaji wa mbegu zisizo katika vifungashio rasmi.
Rai hiyo imetolewa Julai 2, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea banda la Taasisi hiyo lililopo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Chimagu amewahimiza wananchi kutembelea banda la TOSCI ili kupata elimu kuhusu matumizi ya mbegu bora na umuhimu wake katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao.
Amesema TOSCI, ambayo ipo chini ya Wizara ya Kilimo, ina jukumu la kusajili na kudhibiti ubora wa mbegu zote zinazowafikia wakulima ili kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotakiwa na kutoa matokeo bora shambani.
Amesema matumizi ya mbegu bora ni msingi wa kuongeza uzalishaji wa mazao, hivyo taasisi hiyo inaendelea kusimamia ubora wa mbegu ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zinazofaa kulimwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Mbegu yoyote iliyo bora lazima iwe imesajiliwa. Kabla ya kusajiliwa hupitia hatua mbalimbali za majaribio ili kuthibitisha kuwa inafaa kuzalishwa katika mazingira tofauti ya Tanzania na kuwa na sifa bainishi kwa kila zao, iwe ni mahindi, mpunga au mtama,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka msisitizo mkubwa katika kuendeleza kilimo biashara, huku matumizi ya mbegu bora yakitajwa kuwa msingi wa kufanikisha azma hiyo. Amesema mchango wa TOSCI ni kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa tija na mazao yao yanakidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Chimagu amesema Tanzania kwa sasa inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 130, mafanikio ambayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya mbegu bora.
Aidha, amesema juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kufungua masoko mapya zimeongeza fursa kwa wakulima, hivyo ni muhimu kutumia mbegu zilizohakikiwa na TOSCI ili kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania.
Pia amesisitiza kuwa mbegu zote zinapaswa kuuzwa katika vifungashio rasmi vinavyoonesha aina ya mbegu pamoja na kampuni iliyoizalisha, akibainisha kuwa utaratibu huo ni matakwa ya sheria na unalenga kumlinda mkulima dhidi ya matumizi ya mbegu zisizokidhi viwango.

More Stories
Kapinga aipongeza TEMESA kwa mageuzi ya Kidijitali
Wanawake wanufaika zaidi ya Asilimia 51 mikopo SELF
Waziri apongeza NBS kuweka Takwimu Mtandaoni