July 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Kapinga apongeza mafanikio ya TTCL

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika utendaji wake wa kibiashara baada ya kupata faida, kutoa gawio kwa Serikali na kutunukiwa tuzo maalum na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini.

Mafanikio hayo yamepongezwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alipotembelea banda la TTCL katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) leo, ambapo amesema hatua hiyo inaonesha uimara wa shirika hilo na mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.

Kapinga amesema hatua ya shirika hilo kupata faida na kurejesha gawio serikalini ni ishara ya usimamizi mzuri wa rasilimali za umma na utekelezaji wenye tija wa mikakati ya biashara.

Aidha, amesema TTCL inaendelea kukua kwa kasi na kuwa mhimili muhimu katika kuhamasisha uchumi wa kidigitali nchini kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, hususan huduma za mkongo wa taifa na teknolojia za kisasa.

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano kwa Umma wa TTCL, Emerco Mashelle, amemweleza Waziri kuwa uwekezaji katika viwanda vya ndani vya kutengeneza fibre utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za ununuzi wa vifaa kutoka nje ya nchi, hatua itakayowezesha TTCL kuwafikia wateja wengi zaidi nchini.

“Tunawajengea wateja huduma ya fibre bure hadi mlangoni mwao. Uwepo wa viwanda hivi hapa nchini utatusaidia kupata vifaa kwa gharama nafuu, jambo litakalotuwezesha kupanua mtandao na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” amesema.

Amesisitiza kuwa upatikanaji wa vifaa vya mawasiliano vinavyozalishwa nchini ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya mawasiliano na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.