July 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaendelea kuboresha huduma usafi wa mazingira

Na Zena Mohamed, TimesmajiraOline,Dodoma

SERIKALI imejipanga kuhakikisha huduma za usafi wa mazingira zinapatikana kwa wananchi wote kupitia mikakati madhubuti na jumuishi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda afya za wananchi na kuharakisha maendeleo endelevu nchini.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo Julai 2,2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Prof. Paramagamba Kabudi, wakati wa Kongamano la Pili la Kitaifa la Usafi wa Mazingira lililoambatana na uzinduzi wa Mwongozo wa Mipango Jumuishi ya Usafi wa Mazingira wa mwaka 2025.

Prof. Kabudi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka kipaumbele katika kuboresha huduma za usafi wa mazingira ili kuhakikisha zinawafikia wananchi wote.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuona Tanzania inakuwa na miji na vijiji safi, huku akiwataka wananchi kuachana na tabia ya kutupa taka ovyo, hususan kwenye mitaro wakiamini kuwa maji ya mvua yatazisomba.

“Huduma za usafi wa mazingira si suala la uhifadhi wa mazingira pekee, bali ni msingi wa ubinadamu, afya na maendeleo. Tunapaswa kujenga utamaduni wa kupenda na kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Prof. Kabudi.

Aidha, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kulinda mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisema hatua hizo zimechangia kupungua kwa matumizi ya nishati chafu nchini.

Prof. Kabudi pia amesisitiza umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji, kusimamia utekelezaji wa sera na sheria za mazingira pamoja na kuwekeza katika huduma za usafi wa mazingira, akieleza kuwa hatua hizo ni uwekezaji wa moja kwa moja katika afya na maendeleo ya wananchi.

Alitaja changamoto zinazokwamisha usafi wa mazingira kuwa ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, makazi holela, upungufu wa vyoo bora hasa katika masoko, pamoja na ukosefu wa maeneo ya kunawia mikono yenye maji tiririka katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Kunti Majala, aliipongeza EWURA kwa kuandaa kongamano hilo, akisema limetoa fursa ya kujadili namna bora ya kuimarisha usafi wa mazingira nchini.

Naye Mkurugenzi wa Fedha wa EWURA, Stanley Mahembe,amesema takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mamlaka 84 za maji nchini, ni mamlaka 24 pekee zilizokuwa na mipango ya kutibu majitaka na tope kinyesi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweli, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma ipo tayari kutekeleza maelekezo yote yatakayotokana na Mwongozo wa Mipango Jumuishi ya Usafi wa Mazingira ili kuboresha usafi wa mazingira na huduma za afya kwa wananchi.