Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online
WAKULIMA zaidi ya Mil. 1.3 katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Ruvuma wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kidigitali wa utambuzi wa viwango sahihi vya matumizi ya mbolea na afya ya udongo, unaolenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kimkakati ikiwemo mahindi, mpunga na viazi mviringo.
Mradi huo, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia Kituo cha Uyole na Fondation OCP Tanzania, utatekelezwa katika hatua tatu ambazo ni utoaji wa elimu na uanzishaji wa mashamba darasa, upimaji wa afya ya udongo, na uandaaji wa ramani za kidigitali za udongo.
Mtafiti Mwandamizi wa Masuala ya Afya ya Udongo kutoka TARI-Uyole, Fredrick Mlowe, amesema mradi huo unalenga kuwainua wakulima kiuchumi kwa kuwawezesha kupata mapendekezo sahihi ya aina na kiwango cha mbolea kupitia simu za mkononi kulingana na hali ya udongo katika maeneo yao.

Amesema kabla ya kuanza rasmi kwa mfumo huo, watafiti wamefanya majaribio katika maeneo zaidi ya 23 nchini kwa mazao ya mpunga, mahindi na viazi mviringo, sambamba na kuanzisha mashamba darasa 25 kwa ajili ya kuonyesha matumizi sahihi ya mbolea.
Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi wa TARI-Uyole, Dkt. Denis Tippe, amewataka wakulima kutumia mbegu bora na miche yenye umri unaoshauriwa kitaalamu ili kuongeza mavuno.
Amesema matokeo ya mashamba ya majaribio yanaonyesha wakulima waliotumia teknolojia hiyo waliongeza uzalishaji kutoka wastani wa magunia 30 hadi 46 kwa ekari, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 50.
Naye mtafiti wa TARI, Watson Matamwa, amewashauri wakulima kupanda miche yenye umri wa siku 14 hadi 21 na kuweka mbolea ya kupandia ndani ya siku saba baada ya kupandikiza ili mimea iweze kufyonza virutubisho kwa ufanisi.

More Stories
Ndejembi: Bomba la mafuta EACOP lafikia hatua za mwisho
Pedima ang’ara kimataifa,Tuzo za Ubunifu
Kamati ya Bunge yaridhishwa na Mradi wa JNHPP