Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Mbeya
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Ndele Mwaselela, amewataka wasomi wa vyuo vikuu nchini,kutumia elimu na tafiti walizonazo kumtetea kwa hoja Mwenyewe wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, huku wakitanguliza maslahi ya Taifa.
Mwaselela ametoa wito huo Juni 28, 2026, wakati wa sherehe za mahafali ya Seneti ya Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu ya CCM Mkoa wa Mbeya, zilizofanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini hapa.

Amesema wasomi wanapaswa kujibu hoja zinazotolewa dhidi ya Serikali kwa kutumia takwimu, ushahidi na utafiti badala ya kuacha taarifa zisizo sahihi kuendelea kusambaa.
“Tunataka nyinyi wasomi muende mkamtetee Mwenyekiti wetu, Rais Samia, kwa hoja.Mtu akisema tangu aingie madarakani amekopa sana, muulize amefananisha na nini.Kukopa kunaendana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Je, ameangalia miradi yote iliyotekelezwa na Rais Samia?,”amehoji Mwaselela.
Ameeleza kuwa mafanikio ya Serikali yanapaswa kufafanuliwa na wasomi pamoja na viongozi,akitaja utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere, ambalo alisema limepiga hatua kubwa kutoka takribani asilimia 37 hadi kufikia zaidi ya asilimia 90 ya utekelezaji.
Pia ametaja kukamilika kwa miradi mbalimbali ya viwanja vya ndege na uboreshaji wa miundombinu ya vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambayo imebadilishwa kutoka hali ya zamani na kuwa ya kisasa.
“Hayo ndiyo wasomi mkayaseme, msikubali Mwenyekiti wa Taifa, Rais Samia, kubagazwa wakati majibu mnayo. Seneti za vyuo vikuu zikakae, zichambue hoja, zifanye tafiti na zijibu kwa hoja,”amesema.
Sanjari na hayo Mwaselela amesema,Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika elimu ya juu, hivyo ni wajibu wa wasomi kuitumia elimu hiyo kulieleza Taifa mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.
Akizungumzia umuhimu wa amani, amesema maendeleo hayawezi kupatikana bila utulivu,amesisitiza kuwa kila Mtanzania ana jukumu la kulinda amani kwa kuwa ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Seneti ya Vyuo Vikuu Mkoa wa Mbeya, Issa Mwazembe,amesema wasomi wanaunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuimarisha elimu ya juu, hususani kupitia ongezeko la fedha za mikopo kwa wanafunzi.
Amesema kwa mwaka 2021, Rais Samia alikuta bajeti ya mikopo ya elimu ya juu ikiwa sh.bilioni 464, lakini kufikia mwaka 2026 imeongezeka na kufikia sh. bilioni 917.
“Rais Samia ameonesha dhamira ya dhati ya kuwainua vijana kupitia elimu. Tunaamini bajeti ya mikopo itaendelea kuongezeka kutokana na kipaumbele anachokitoa kwa maendeleo ya vijana wa Tanzania,”amesema Mwazembe
Naye Katibu wa Seneti ya Vyuo Vikuu Mkoa wa Mbeya, Irene Njiku, akisoma risala kwa mgeni rasmi amesema, Seneti hiyo imefanikiwa kusajili matawi 40 katika mfumo wa vyuo vya kati na vyuo vikuu mkoani Mbeya.


More Stories
Rais Samia kufungua Mkutano wa TMIC 2026
Watakiwa kutimiza wajibu waoÂ
Yas Business,FTCC wawajengea uwezo Wajasiriamali