Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
Yas Business kwa kushirikiana na French-Tanzania Chamber of Commerce (FTCC) imezindua mpango wa SME Masterclass Series wenye lengo la kuwajengea uwezo wamiliki wa biashara ndogo na za kati (SMEs) pamoja na biashara changa (startups) ili kukuza ushindani na matumizi ya teknolojia katika biashara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa mauzo kitengo cha Yas Business anayeshughulikia sekta ya SMEs, Gabriel Ndobho amesema mafunzo hayo yatawapa wafanyabiashara maarifa ya kusimamia biashara kwa ufanisi, kutafuta masoko, kuboresha mifumo ya uendeshaji na kutumia teknolojia kuongeza tija na ukuaji wa biashara zao.

Ndobo ameongeza kuwa Yas Business inaendelea kutoa suluhisho mbalimbali za kidijitali kwa wafanyabiashara, ikiwemo huduma ya Money Box, zinazorahisisha uendeshaji wa biashara na kusaidia ukuaji wa biashara kupitia matumizi ya teknolojia.
Kwa upande wake, mwakilishi wa kampuni ya vifaa vya umeme, Thony Godfrey, amesema programu hiyo imekuwa jukwaa muhimu la kujifunza na kubadilishana uzoefu kati ya wafanyabiashara kutoka sekta mbalimbali. Alisema ushiriki katika mafunzo hayo unawapa fursa ya kujenga mtandao wa kibiashara, kujifunza mbinu mpya za uendeshaji wa biashara na kushirikiana na kampuni nyingine katika kukuza biashara zao.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo, Gloria Amuro, amesema amejifunza kuwa mtu hatakiwi kusubiri kuwa na mtaji mkubwa ndipo aanzishe biashara, bali anaweza kuanza na rasilimali alizonazo huku akiendelea kukuza biashara hatua kwa hatua.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa umuhimu wa kufanya uchambuzi wa soko, kutambua washirika sahihi wa biashara, kubuni bidhaa au huduma zenye ushindani na kutumia majukwaa ya kidijitali kujitangaza na kuongeza mauzo.
Gloria amesema elimu hiyo itawasaidia wajasiriamali kutumia mitandao ya kijamii na teknolojia kama nyenzo muhimu za kukuza biashara na kuongeza mapato.

More Stories
Ziara ya Rais Samia Urusi yaleta fursa mpya
Msigwa:Kiwango uchumi wa kujitegemea kimeongezeka nchini
Ndejembi:Miradi mikubwa kuipa nguvu Gridi ya Taifa