June 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndejembi:Miradi mikubwa kuipa nguvu Gridi ya Taifa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira

Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha Gridi ya Taifa kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya njia za. kusafirisha umeme, inayotarajiwa kuongeza uwezo, uthabiti na usalama wa mfumo wa umeme nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Kituo cha Usimamizi wa Mfumo wa Gridi ya Taifa jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb), amesisitiza umuhimu wa kukamilisha kwa wakati miradi ya njia za kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400, ikiwemo Chalinze–Kinyerezi na Chalinze–Dodoma, akieleza kuwa ndiyo msingi wa kuendelea kuimarisha Gridi ya Taifa na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na sekta za uzalishaji.

“Kukamilika kwa miradi ya njia za kusafirisha umeme za msongo wa kilovoti 400 ni hatua muhimu katika kuimarisha Gridi ya Taifa. Serikali haitakuwa tayari kuona miradi hii inachelewa kwa kuwa ndiyo msingi wa upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na kwa maendeleo ya uchumi wa nchi,” amesisitiza.

Sambamba na utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati, Waziri Ndejembi ameiagiza TANESCO kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi na udhibiti wa Gridi ya Taifa ili hitilafu zinazoweza kujitokeza katika eneo moja zisiwe na athari kwa mfumo mzima wa usambazaji wa umeme nchini.

Aidha, kufuatia hitilafu iliyojitokeza katika Gridi ya Taifa Juni 27, 2026 na kusababisha kukosekana kwa huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo nchini, Waziri ameagiza kuundwa kwa kamati ya uchunguzi itakayojumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama ili kubaini chanzo cha hitilafu hiyo na kupendekeza hatua za kudumu za kuzuia matukio kama hayo kujirudia. Kamati hiyo imeelekezwa kuwasilisha taarifa ya awali ndani ya wiki moja.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema Wizara itasimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri, ikiwemo kazi ya kamati ya uchunguzi na utekelezaji wa miradi ya kuimarisha Gridi ya Taifa.

“Tutaimarisha usimamizi wa utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri na kufuatilia kwa karibu miradi ya njia za kusafirisha umeme ili ikamilike kwa wakati, hatua itakayoongeza uthabiti na ufanisi wa Gridi ya Taifa,” amesema Mhandisi Mramba.

Hatua hizo zinaakisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya umeme nchini, kwa lengo la kuongeza uthabiti wa Gridi ya Taifa, kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa.