Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza,limeonya na kupiga marufuku magari ya shule yenye vioo vya giza(tinted) kutokubeba wanafunzi.
Huku jeshi hilo mkoani Mwanza limefanikiwa kukagua magari 25 ya shule katika zoezi la ukaguzi wa magari hayo lililoanza Juni 18,2026,kwa lengo la kuboresha huduma ya usafiri na kuimarisha usalama wa wanafunzi.

Zoezi hilo lililozinduliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbrod Mutafungwa Juni 18,2026 limeendelea hadi , Juni 26, 2026, katika uwanja wa shule ya msingi Nyang’homango wilayani Misungwi mkoani hapa.
Akizungumza Juni 26,2026 na madereva pamoja na walezi wa wanafunzi wakiwemo “patron na matron”,Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Misungwi, ASP. Maris Isomba, amesema kuwa lengo kuu la ukaguzi huo ni kuhakikisha watoto wanakuwa salama wanapokwenda na kurudi kutoka shuleni.
ASP. Isomba amekemea tabia ya baadhi ya wamiliki wa magari ya shule kuweka vioo vya giza (tinted). Amesema kitendo hicho ni kinyume cha sheria kwa magari ya usafiri wa umma na yanayobeba wanafunzi kwani kinaweza kuchochea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
”Magari ya shule yanatakiwa kuwa na vioo angavu ili kuruhusu mtu yeyote kuona mazingira ya ndani na kuhakikisha watoto wako salama,”amesisitiza ASP. Isomba.
Pia ametoa wito kwa wamiliki ambao bado hawajapeleka magari yao yakakaguliwe kuhakikisha wanatimiza takwa hilo la kisheria ambapo amewaonya watakaokaidi,kwani watafuatwa kwenye maeneo ya shule zao huku magari yatakayobainika kuwa mabovu yatapigwa marufuku kutoa huduma hadi yarekebishwe na kukaguliwa tena.
Kwa upande wake Sajenti Juliana Nyambuka, kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Misungwi, amewataka madereva na walezi hao kuwalinda watoto na kuzuia vitendo vya ukatili wawapo kwenye vyombo vya usafiri.
”Ukatili wa kijinsia ni sawa na mauaji mtoto akishalawitiwa, maisha yake yote yanakuwa yameharibiwa,”amesema Sajenti Juliana.
Nao madereva na wasimamizi wa magari hayo akiwemo Pascal Charles amesema,ukaguzi huo unawakumbusha kutekeleza wajibu wao na kubaini mapungufu yaliyopo kwenye magari yao,hivyo jambo hilo ni zuri na wanalifanyia kazi.
Dereva Sadiki Damasi amesema,elimu hiyo itawasaidia katika matengenezo na urekebishaji wa magari yao hivyo alishukuru kwa juhudi hizo zilizofanya na askari wa Misungwi.
“Kwa kweli nimepata elimu nzuri ya kuwa makini na kuwalinda watoto wasifanyiwe ukatili wa kijinsia. Nawaomba madereva wenzetu wazingatie sheria ili kulinda watoto na watumiaji wengine wa barabara,”amesema Matron Cothorata.


More Stories
NBS yawakumbuka wafungwa Isanga
Mix yaendelea kugawa Mamilioni
Katambi atangaza kusitishwa vibali vya mikutano ya Siasa