


Na Joyce Kasiki,Timesmjaira online,Dodoma
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeendelea kuimarisha ushirikiano na Jeshi la Magereza nchini kwa lengo la kuboresha ukusanyaji wa takwimu, kufanya tafiti zinazosaidia kupunguza kurejea kwa wafungwa magerezani, pamoja na kuboresha ustawi wa wafungwa na mahabusu kupitia msaada wa kijamii.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa wafungwa leo Juni 26,2026Â katika Gereza Kuu la Isanga, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt.Amina Msengwa, amesema ushirikiano huo umeiwezesha NBS kuzalisha takwimu rasmi za magereza zinazokidhi viwango vya kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2023 hadi 2025.
Amesema taarifa ya takwimu za magereza ya mwaka 2025 ilitolewa mwezi Machi 2026, jambo linalodhihirisha ufanisi wa Jeshi la Magereza katika ukusanyaji na uwasilishaji wa takwimu kwa wakati.
Mbali na uzalishaji wa takwimu, Msengwa alisema NBS inaendelea na utafiti ulioanza mwezi Machi mwaka huu unaochunguza sababu zinazowafanya baadhi ya wafungwa kurejea tena magerezani baada ya kumaliza vifungo vyao.
Ameeleza kuwa matokeo ya utafiti huo yataisaidia Serikali na wadau mbalimbali kupanga mikakati ya kuwawezesha wafungwa wanaomaliza vifungo kupata ujuzi, mazingira rafiki na fursa zitakazowasaidia kujenga maisha mapya bila kurudia makosa yaliyowapeleka gerezani.
Dkt.Msengwa amesema NBS pia imeona umuhimu wa kuonesha upendo kwa wafungwa na mahabusu kwa kutoa msaada katika Gereza la Isanga kwa wafungwa kwani nao ni sehemu ya jamii hivyo wanahitaji faraja.
Amewaasa wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza katika kuboresha mazingira ya wafungwa na mahabusu, huku akilipongeza jeshi hilo kwa huduma na malezi linayotoa kwa watu waliopo magerezani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza Kuu la Isanga, ASP William Saleta Makwaya, ameishukuru NBS kwa msaada huo akisema utasaidia kuboresha shughuli mbalimbali za gereza pamoja na kuimarisha ushirikiano katika ukusanyaji wa takwimu na tafiti kuhusu wafungwa wanaorudia makosa.
Amesema Jeshi la Magereza linaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na stadi mbalimbali kwa wafungwa na mahabusu ili wanapotoka magerezani wawe na uwezo wa kujitegemea na kupata ajira, hatua inayolenga kupunguza vitendo vya kurejea tena gerezani.
ASP Makwaya amebainisha kuwa changamoto kubwa inayochangia wafungwa kurejea magerezani ni namna wanavyopokelewa na jamii baada ya kumaliza vifungo vyao.
Ameoa wito kwa jamii kuwapokea, kuwaunga mkono na kuwawezesha wafungwa waliomaliza vifungo kuanza maisha mapya badala ya kuwanyanyapaa, akisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza uhalifu na kujenga jamii salama.

More Stories
Magari yenye ‘tinted’ marufuku kubeba wanafunziÂ
Mix yaendelea kugawa Mamilioni
Katambi atangaza kusitishwa vibali vya mikutano ya Siasa