June 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uvccm Mtwara yasisitiza Ulinzi wa Amani

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mtwara limepitisha maazimio mbalimbali ya kisiasa na maendeleo yenye lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa, amani na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030.

Maazimio hayo yamepitishwa katika kikao cha kawaida cha Baraza kilichofanyika mkoani Mtwara tarehe 25 Juni 2026.

Katika kikao hicho, wajumbe wa Baraza walimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake na juhudi anazoendelea kuzifanya katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini, ikiwemo Mkoa wa Mtwara.

Baraza hilo pia limepongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, utulivu na usalama. Wajumbe walivitaka vyombo hivyo kuendelea kusimamia sheria na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha mshikamano na amani ya Taifa.

Aidha, Baraza limewahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwa manufaa ya Taifa.

Kuhusu suala la maboresho ya Katiba, Baraza limeeleza kuwa ni sehemu ya ajenda ya Chama na Serikali na kwamba linapaswa kuendelea kushughulikiwa kwa kuzingatia taratibu na mipango iliyowekwa.

Vilevile, UVCCM Mkoa wa Mtwara limewataka vijana kuendelea kulinda umoja wa kitaifa, kuimarisha mshikamano na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuchochea ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Baraza hilo limebeba kaulimbiu isemayo, “Kulinda na Kujenga Umoja.”