June 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbeya yapokea magari mapya

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbeya imepokea magari mawili mapya aina ya Land Cruiser Hardtop yenye milango mitano na uwezo wa kubeba watu 10 kila moja kwa ajili ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na kitengo cha mipango na uratibu.

Magari hayo yenye thamani ya Sh Mil 461.8 yamenunuliwa kwa fedha kutoka serikali kuu na mapato ya ndani ya halmashauri, yakilenga kuimarisha utendaji wa watumishi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa magari hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amesema upatikanaji wa magari hayo utaongeza uwezo wa halmashauri katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aidha, amesema mchango wa mapato ya ndani ya Halmashauri umewezesha kukamilika kwa ununuzi huo na kwamba magari hayo yanatarajiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya, Aidda Haule, amesema ni muhimu magari hayo yakatumike kwa malengo yaliyokusudiwa na yatunzwe ili yaendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Erica Yegella, amesema ununuzi wa magari hayo umefanikiwa kupitia ushirikiano wa Serikali Kuu na mapato ya ndani ya Halmashauri.

Amesema magari hayo yataimarisha usimamizi wa miradi, kuongeza ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia divisheni husika.