June 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM Songwe waivaa Chadema yadai Rais hapatikani kwa porojo za mtandaoni

Na Mwandishi Wetu, Mbozi.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe kimesema kuwa, nafasi ya urais haiwezi kupatikana kwa porojo za mitandaoni, propaganda za kisiasa au malalamiko yasiyo na ushahidi, bali kupitia mchakato wa kidemokrasia wa uchaguzi unaowapa wananchi nafasi ya kufanya uamuzi wao.

Kauli hiyo imetolewa Juni 25, 2026 na Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Songwe, Yusuph Ally Rajab, wakati akizungumza na waandishi wa habari kujibu madai yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Songwe, Isakwisa Lupembe, kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na CCM walishinda uchaguzi Mkuu uliopita kwa msaada wa jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola.

Rajab amesema Lupembe alitoa madai na tuhuma hizo, Juni 24, 2026 katika mkutano wa hadhara wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, John Heche, uliofanyika Tunduma, Wilaya ya Momba.

Akijibu tuhuma hizo, Rajab amesema madai ya kuhusisha ushindi wa Rais, CCM na vyombo vya dola ni sehemu ya propaganda za kisiasa zinazolenga kuficha udhaifu wa chama hicho, ambacho alidai hakikujipanga ipasavyo katika uchaguzi uliopita na kukimbia uchaguzi huo kwa hila.

“Rais hapatikani kwa porojo za mitandaoni wala propaganda za kisiasa, bali Rais hupatikana kwa kura za wananchi kupitia uchaguzi unaofanyika kwa mujibu wa sheria za nchi,” amesema Rajab.

Amesema ushindi wa CCM unatokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, miradi ya maendeleo inayotekelezwa na imani ambayo wananchi wameendelea kuiweka kwa chama hicho kwa miaka mingi.

Rajab amedai kuwa badala ya kutafuta visingizio baada ya uchaguzi, Chadema inapaswa kuimarisha sera zake, kujijenga kisiasa na kutafuta ridhaa ya wananchi kupitia sanduku la kura.

Aidha, amewataka viongozi wa Chadema kuhakikisha wanatoa kauli zinazozingatia ukweli, takwimu na ushahidi, badala ya kutoa tuhuma ambazo hazijathibitishwa.

Amesema siasa za ushindani zinapaswa kujengwa katika hoja na sera zinazowagusa wananchi, huku akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanapatikana kupitia mshikamano, amani na kuheshimu misingi ya demokrasia.

Rajab amehitimisha kwa kusema CCM itaendelea kuomba ridhaa ya wananchi kwa njia za kidemokrasia na kuendeleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya Watanzania.