June 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yaongeza Wataalamu wa kulinda Amani Kimataifa

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa baada ya wahitimu 22 wa mafunzo maalum ya walinda amani wa kiraia kuhitimu mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za kisasa za migogoro duniani.

Akifunga mafunzo hayo ya juzi jijini Dar es Salaam, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Haji Othman alisema mazingira ya sasa ya operesheni za kulinda amani yanahitaji wataalamu wenye uelewa mpana unaovuka masuala ya kijeshi na kiusalama pekee.

Amesema migogoro ya sasa imekuwa ikichochewa na sababu mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa, hali inayohitaji wataalamu wenye uwezo wa kushughulikia changamoto hizo kwa ufanisi.

“Operesheni za kulinda amani zimekuwa ngumu zaidi kuliko ilivyokuwa zamani. Hivyo, tunahitaji wataalamu wenye maarifa na uwezo wa kufanya kazi katika mazingira yenye changamoto nyingi,” amesema.

Mafunzo hayo yalifadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kwa kushirikiana na Serikali ya Japan na yalihusisha washiriki kutoka Tanzania, Malawi, Namibia na Zimbabwe.

Washiriki walipatiwa mafunzo katika maeneo mbalimbali ikiwemo usimamizi wa migogoro, sheria za kimataifa za operesheni za amani, masuala ya jinsia, ushirikiano kati ya raia, polisi na jeshi pamoja na huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia.

Kwa mujibu wa Luteni Jenerali Othman,amesema. mafunzo hayo yataongeza idadi ya wataalamu wa kiraia wenye sifa za kushiriki katika misheni za Umoja wa Mataifa na kuimarisha uwezo wa Tanzania kuandaa wataalamu wa kushiriki katika maeneo yenye migogoro duniani.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema wahitimu hao sasa wako katika nafasi nzuri ya kushiriki katika shughuli za kulinda amani, usuluhishi wa migogoro, misaada ya kibinadamu na juhudi za maendeleo katika maeneo yanayokumbwa na migogoro.

Amesema mafanikio ya mafunzo hayo yanaakisi ushirikiano imara kati ya Tanzania, Japan na Umoja wa Mataifa katika kujenga uwezo wa wataalamu wa kiraia, polisi na wanajeshi wanaohitajika katika operesheni za kimataifa.

Mwakilishi wa Serikali ya Japan amesema nchi hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuandaa wataalamu wa kulinda amani, akibainisha kuwa amani na usalama wa binadamu ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu duniani.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema yamewapa uelewa mpya kuhusu nafasi ya raia katika kulinda amani na namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuzuia na kutatua migogoro ndani na nje ya nchi.

Mafunzo hayo yanaendelea kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa miongoni mwa nchi zinazoandaa wataalamu wenye viwango vya kimataifa kwa ajili ya operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.