Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
BARAZA la Sanaa la Tanzania (BASATA) limesema, linajukumu kubwa la uzalishaji wa kazi za Sanaa pamoja na kuhakikisha ushiriki wa jamii katika kazi hizo ili kukuza maendeleo ya sekta ya sanaa nchini na kusisitiza wasanii kuwa makini wakati wa ujazaji mikataba yao.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza wakati wa warsha ya siku moja ya kuboresha mahusiano kati ya Waandishi wanaoandika habari za sanaa na utamaduni ambao pia ni wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza MPC na Basata iliofanyika Jijini Mwanza.
Mngereza amesema, Basata inajukumu la kuhakiksha sekta ya sanaa inasonga mbele ila kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wasanii juu ya ujazaji wa mikataba na mapromota na amewasisitiza wasanii kuwa makini wakati wa ujazaji wa mikataba hiyo au kuwashirikisha wataalamu ili kuweza kupata haki zao stahiki kupitia mikataba ambapo huduma hiyo inatolewa bure baraza hilo.
Amesema kuwa, kila mahali sanaa zipo na zisizotenganishwa ili kuondokana na changamoto hiyo na kuleta nuru na mafanikio kwa wasanii na ndio maana huduma hiyo inatolewa bure na BASATA hivyo wasanii waitumie fursa hiyo ipasavyo kwani ofisi yake na maofisa wapo tayari kufanya kazi na wadau wa sanaa.
“Jukumu letu kubwa ni kufufua na kukuza maendeleo ya sanaa nchini, uzalishaji wa kazi za sanaa pamoja na kuhakiki ushiriki wa jamii katika kazi za sanaa natunafanya kazi kwa ukaribu zaidi na COSOTA, Bodi ya Filamu nchini, BAKITA na TCRA kwa lengo la kuhakikisha kazi za wasanii zinalindwa,” amesema Mngereza.
Pia amesisitiza kuwa, Baraza hilo halimuogopi msanii yeyote yule na hawamuonei mtu bali wanasimamia sheria, taratibu, kanuni na miongozo katika kuchukua hatua pia wanatoa elimu kwa wasanii kutumia mitandao kwa usahihi na kujiingia vipato zaidi ili kukuza ubunifu katika kazi za sanaa na ubora wa kazi na limekuwa na utaratibu wa kukutana na waandishi katika Kanda mbalimbali ili kueleza kazi zao kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko amesema, kazi ya uandishi wa habari inakuwa siku hadi siku hivyo elimu hiyo itawaongezea ueledi ili waweze kuandika habari zao vizuri hivyo aliwataka kutumia kalamu zao vyema kwa uandika habari zenye weledi kwa kuwasilisha vilio vya wasanii hususani wale wachanga ili kukuza ndoto zao kwani sanaa inaweza kuchangia pato la uchumi wa nchi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja.
Hata hivyo baadhi ya washiriki wa warsha hiyo walitoa mapendekezo yao na maoni yao ikiwemo suala la BASATA kufungua ofisi kila Mkoa ili kusogeza huduma karibu na walengwa.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025