June 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Makongoro akutana na Noble Helium kujadili maendeleo ya mradi wa gesi, Rukwa



‎Na Israel Mwaisaka Rukwa.

‎Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,  Charles Makongoro Nyerere,  amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Kampuni ya Noble Helium nchini Tanzania,  Joseph Uisso, kuhusu maendeleo ya mradi wa gesi ya helium unaotekelezwa katika Mkoa wa Rukwa.

‎Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa yamelenga kujadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo pamoja na manufaa yanayotarajiwa kupatikana kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi, hususan katika vijiji vya Kisa na Zimba, vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.

‎Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zimejadiliana kuhusu mchango wa mradi huo katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo husika, ikiwemo fursa za ajira, ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za mradi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii.

‎Makongoro amesisitiza umuhimu wa uwekezaji huo kuendelea kuwanufaisha wananchi wa Mkoa wa Rukwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya nchi, huku akieleza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha utekelezaji wa mradi huo kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

‎Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Noble Helium, Joseph Uisso, alieleza dhamira ya kampuni hiyo kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na jamii inayozunguka eneo la mradi ili kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo chanya na endelevu kwa wananchi na uchumi wa nchi.