




Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Iringa
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amewataka wananchi kuwakataa wanasiasa wanao hamahama vyama na kumuita aliyekuwa Mbunge wa CHADEMA, Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kuwa ni Kanjanja wa siasa.
Pia, amesema wapo wanasiasa wenye tabia ya kukilalamikia na kukisema vibaya chama alichokuwa mwanzo pindi anapokuwa amehamia kwenye chama kingine baada ya kukosa cheo.
Kihongosi ameyasema hayo Juni 20, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwembetogwa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, ambapo kupitia mkutano wake wa hadhara, alionesha video ya kipindi cha kampeni, kipindi ambacho Msigwa alihamia CCM akionekana akimsifu Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kuueleza Umma kuwa CCM ndiyo chama chenye sera, ambapo Kihongosi alisema kauli za sasa za Msigwa zinakinzana na alichokuwa akisema alipohamia CCM.
Akizungumza mbele ya wananchi na wanachama wa CCM, Kihongosi alidai kuwa Msigwa ni miongoni mwa viongozi wanaobadilisha misimamo yao ya kisiasa mara kwa mara kulingana na mazingira yanavyobadilika.
Katika mkutano huo, Kihongosi aliwaomba wananchi kusikiliza kwa makini kabla ya kuonyesha video hiyo ya Msigwa alipokuwa amehamia CCM na kuhutubia katika majukwaa ya chama hicho maeneo mbalimbali nchini.
Katika video hiyo ya wakati wa kampeni za CCM katika uchaguzi mkuu 2026, Msigwa alisikika akisema kuwa CCM iko katika mikono salama chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kwamba chama hicho kina sera zinazolenga maendeleo ya wananchi.
Baada ya video hiyo kuchezwa, Kihongosi alisema ushahidi huo unaonyesha wazi kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa hawasimamii misimamo yao kwa uthabiti na hubadilika kulingana na maslahi yao.
“CCM haiwezi kuyumbishwa na kauli za viongozi wanaokihama chama hicho na baadaye kukirejea au kukikosoa hadharani,” alisema Kihongosi na kuongeza kuwa
“CCM inaendelea kuaminiwa na wananchi na itaendelea kufanya kazi za maendeleo bila kujali hoja zisizofaa za kisiasa kutoka kwa wapinzani wake,”
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Richard Kasesela, alishangazwa na viongozi wa CHADEMA waliofika mkoani hapo kufanya mkutano kudai kwamba hakuna kilichofanyika.
“Walikuja hapa na wakashuka kwa ndege ya Air Tanzania katika uwanja wa ndege Nduli alafu wanasema hakuna kinachofanyika, hawa kweli ni makwelekwele,” alisema Kasesela na kuongeza kuwa
“Kuna mmoja alikuja CCM akakimbia baada ya kukosa cheo na huyu amekosa cheo kwa sababu baada ya kuangalia wasifu wake tumebaini hana sifa ya kuwa hata Katibu Kata,”
Aidha mwandishi wa gazeti hili, ili kusikia kuhusu madai hayo, alifanya jitihada za kumtafuta Mchungaji Peter Msigwa ambaye alisema, hakuwa katika sehemu nzuri ya kuongelea suala hilo na kusema kuwa atakapopata nafasi ataangalia kama kuna umuhimu wa kujibu madai hao au lah.
“Sipo sehemu nzuri kwa sasa lakini pia sijasikiliza huo mkutano ingawa najua Kenani yupo hapa Iringa anafanya mkutano, hivyo nikipata muda wa kusikiliza huo mkutano ndio nitamjibu kama kutakuwa na umuhimu wa kumjibu,” alisema Msigwa
Aidha akijibu suala la yeye kukataliwa na Wananchi na wanachama katika mkutano wa Chadema uliofanyika Iringa hivi karibuni, Msigwa alisema si kweli kuwa alikataliwa na Wananchi na hizo ni ndoto.

More Stories
FCC YAANZA KLABU SHULENI KUJENGA ELIMU USHINDANI
TBA yajenga nyumba bei nafuu nchi nzima
Ngoma Festival ilivyotikisa Rukwa,fursa za Mwenge zaanikwa