June 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MCB yasisitizwa mambo sita Dira 2050

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

MWALIMU Commercial Bank(MCB)imesisitizwa mambo 6, katika kuhakikisha inatoa mchango na kushirikishi kufanikisha  utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya  2050 huku dhamira ya Serikali ni kuhakikisha benki hiyo inaendelea kusimama ili kuendelea kutoa fursa mbalimbali za uchumi.

Hayo yameelezwa leo Juni 18,2026 na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira na Mahusiano Deus Sangu, wakati akifungua mkutano mkuu wa 10,wa MCB,uliofanyika jijini Mwanza.

Ambapo ameikumbusha MCB inaposherekea miaka 10, kuwa ni wakati sahihi kwani  utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 unaanza,na ili benki hiyo  ishiriki ipasavyo katika utekelezaji wa dira hiyo yapo mambo ya kuzingatia,ikiwemo kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha,kwa kuweka  mpango mkakati wa kuongeza huduma za mikopo na bidhaa za kifedha kwa walimu, vijana, wanawake na wafanyabiashara wadogo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

Pia kusaidia uwekezaji katika elim kwani walimu  ni sehemu kubwa ya wamiliki wa benki na ni nguzo muhimu ya maendeleo ya rasilimali watu.Hivyo benki inaweza kuweka mikakati ya kuendeleza mikopo ya elimu, ujenzi wa nyumba za walimu na miradi inayoboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Sangu amesema,benki inapaswa kukuza uchumi wa kidijitali,kwani Dira 2050 inasisitiza matumizi ya teknolojia na ubunifu. Hivyo ijikite katika kuimarisha huduma za kidijitali, kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kisasa.

Aidha kuwezesha ujasiriamali na viwanda,kupitia mikopo na huduma za ushauri wa biashara,kwa benki hiyo  kuweka mikakati ya kusaidia maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati pamoja na kuongeza thamani ya mazao, jambo ambalo ni msingi wa uchumi wa viwanda unaolengwa na Dira 2050.

Vilevile kukuza utamaduni wa kuweka akiba na uwekezaji kwa  kutoa bidhaa zinazowahamasisha wananchi kuweka akiba na kuwekeza,kwani benki hiyo  inaweza kuongeza mtaji wa ndani unaohitajika katika kufanikisha miradi ya maendeleo ya taifa.

Pamoja na kuwekeza katika miradi yenye tija na maendeleo endelevu,ambapo  inaweza kushiriki kufadhili sekta za kilimo, nishati,nyumba, afya na miundombinu ambayo ni muhimu katika kufikia uchumi imara na ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa MCB,Richard Makungwa,amesema kama benki wana dira  yao ya miaka mitano 2026-2030,inayoakisi kwa kiwango kikubwa Dira ya Taifa ya 2050,ambapo lengo ni kuboresha utoaji huduma kidigitali na kuboresha utoaji wa fedha na  elimu.

“Pia tutajikita katika utoaji mikopo ya kilimo,tunaubia na benki ya kilimo,tumejikita pia kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati na hatujawaacha walimu, hawa ndio msingi wa benki na wateja wetu.Kama benki tunafanya shughuli  zote za kibenki na kauli mbiu ni kuweza kufikia wateja wote na wananchi ili kufanikisha Dira ya Taifa ya 2050,”.

Mmoja wa wanahisa wa benki hiyo,Mwl.Masau Bwire,amesema Walimu wana mchango wa kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa kupitia benki hiyo,kama ambavyo Waziri alivyoelekeza  mambo sita inayopaswa kuzingatia.

“Miongoni mwa mambo hayo muhimu ni kuongeza wigo wa hupatikanaji wa fedha, hapo ndipo  tumeguswa walimu kwenda kufungua akaunti na kuitumia benki hiyo kukopa ili kuboresha kipato chetu sisi  na uchumi wetu uweze kuimarika na kuwa bora kupitia benki hiyo,”amesema Mwl. Bwire.

Benki hiyo mpaka sasa ina wanahisa ambao ni walimu takribani 217,000,pia kuna wanahisa mmoja mmoja ambao siyo walimu ni takribani asilimia 16, ikiwemo benki na mashirika makubwa.