Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbeya
TAASISI ya Tulia Trust imeanza ujenzi wa nyumba mpya kwa ajili ya Queen Andembwisye, mkazi wa Mtaa wa Tonya, Kata ya Ilomba jijini Mbeya, baada ya nyumba yake kubomoka kufuatia mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali na kumuacha yeye pamoja na familia yake bila makazi salama.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Mtaa wa Tonya, mwakilishi wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Tulia Trust, Hady Kalinjila, amesema taasisi hiyo imechukua hatua za haraka kufuatia maelekezo ya Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt. Tulia Ackson, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Uyole.
Amesema tangu familia hiyo ipatwe na mkasa huo imekuwa ikiishi katika mazingira magumu, huku changamoto za makazi, chakula na mahitaji mengine muhimu zikiendelea kuikabili.
“Tulibaini kuwa familia hii haikuhitaji msaada wa makazi pekee, bali pia inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa chakula na mahitaji mengine ya msingi. Mama huyu hana kazi ya kudumu na hutegemea vibarua vya hapa na pale ili kujikimu,” amesema Kalinjila.
Ameongeza kuwa familia hiyo ina watoto watatu wanaosoma shule, akiwemo mmoja wa sekondari na wengine wa shule ya msingi, hali inayoongeza mzigo wa mahitaji ya kila siku.
“Kupitia maelekezo ya Dkt. Tulia Ackson, tumeleta vifaa vya ujenzi na kuanza rasmi ujenzi wa nyumba hii. Vifaa vilivyofikishwa ni pamoja na saruji, mchanga, nondo na matofali ili kuhakikisha familia hii inapata makazi bora na salama,” ameeleza
Andembwisye anaishi na watoto wake watatu pamoja na mama mkwe wake, hivyo kufanya familia hiyo kuwa na watu watano. Nyumba yao ya awali iliharibiwa kutokana na uchakavu uliosababishwa na mvua na upepo mkali.
Kupitia mpango wa “Tulia Trust Mtaani Kwetu,” taasisi hiyo imefanikiwa kujenga nyumba 25 kwa familia zenye mazingira magumu katika maeneo mbalimbali. Ujenzi wa nyumba ya Andembwisye utaongeza idadi hiyo kufikia nyumba 25 zilizojengwa chini ya mpango huo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Tonya, Leonard Japhet, aliishukuru Tulia Trust kwa msaada huo, akibainisha kuwa viongozi wa mtaa wamekuwa wakijitahidi kusaidia familia hiyo kwa kadri ya uwezo wao tangu ilipopata tatizo hilo.
Naye Chifu wa Mtaa wa Tonya, Japhet Ndele, alisema hatua ya Tulia Trust imeonesha moyo wa kujitolea wa Dkt. Tulia Ackson katika kuwasaidia wananchi wenye mahitaji maalum bila ubaguzi.
“Kupitia matendo haya, tumeshuhudia namna Dkt. Tulia alivyo karibu na wananchi na jinsi anavyojitolea kusaidia watu wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha,” amesema Ndele.
Ujenzi wa nyumba hiyo unatarajiwa kurejesha matumaini kwa familia ya Bi. Andembwisye na kuwapatia makazi salama baada ya kipindi kigumu walichokipitia.


More Stories
Wasomi wahimizwa kuelimisha jamii na kulinda Taswira
Rabia: CCM inathamini kila jasho la Mtanzania
NMB yapeleka elimu ya fedha kwa vijana