June 12, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jubilei ya Miaka 50 ya Sabasaba,Nchi 23 kushiriki

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

MKUU wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amesema ameridhishwa na maandalizi ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama SabaSaba, yanayotarajiwa kuanza rasmi Juni 28 mwaka huu, huku akitoa wito kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho hayo ya kihistoria yanayotimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Mapunda alitoa kauli hiyo Juni 12 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika viwanja vya maonesho, ambapo amesema maandalizi yanaendelea vizuri na yanaendana na hadhi ya maadhimisho ya jubilei ya miaka 50 ya Sabasaba.

Amesema maonesho ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee kwa kuwa yatatoa fursa kwa wananchi kujionea maendeleo katika sekta za biashara, uwekezaji na utalii, sambamba na kusherehekea historia ya maonesho hayo ambayo yamekuwa chachu ya maendeleo.

Aidha, Mapunda amezitaka taasisi na ofisi zote za Serikali kuhakikisha mabanda yao yanakamilika ifikapo Juni 20 ili wageni na washiriki watakaofika kwenye maonesho hayo washuhudie maandalizi bora yanayoakisi hadhi ya maadhimisho hayo muhimu.

Kwa upande wake, Dkt Latifa Khamis Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade),amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha maonesho ya mwaka huu yanakuwa makubwa na ya aina yake kwa kutoa fursa za biashara, uwekezaji, burudani na kujifunza kwa wananchi, wazalendo na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Amesema hadi sasa nchi 23 zimethibitisha ushiriki wao katika maonesho hayo, huku makampuni 256 ya kimataifa yakionesha nia ya kushiriki na zaidi ya makampuni 2,776 ya ndani yakijiandikisha kushiriki, jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani na fursa za kibiashara kwa washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, maonesho hayo yatapambwa na programu mbalimbali zikiwemo “Usiku wa Kash Kash”, matembezi maalumu ya kuhamasisha matumizi ya bidhaa za Made in Tanzania pamoja na hafla ya Golden Jubilee itakayofanyika Julai 7 kwa ajili ya kutambua na kuwatunuku wadau waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Maonesho ya Sabasaba kwa kipindi cha miaka 50.