



Na Mwandishi Wetu
BODI ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imefanya mazungumzo na Kampuni ya Egyptian Holding Company for Silos and Storage (EHCSS) ya nchini Misri ili kuimarisha usimamizi wa ghala, matumizi ya teknolojia za kisasa na kukuza biashara ya bidhaa za kilimo kati ya Tanzania na Misri.
Mazungumzo hayo yamefanyika Juni 11, 2026 kati ya ujumbe wa WRRB ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Asangye Bangu, akiongozana na Meneja wa Mipango Tafiti na Bunifu, Fidelis Temu na Afisa Ubora Anatolius Kabyemela na viongozi wa EHCSS wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Dkt.Ashraf Shedeq.
Katika kikao hicho, WRRB imeeleza uzoefu wa Tanzania katika utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, huku EHCSS ikieleza namna inavyosimamia ghala za kisasa za kuhifadhi nafaka kwa kutumia teknolojia zinazosaidia kulinda ubora, usalama na ufanisi wa mazao.
Pamoja na hayo, Ujumbe wa WRRB pia umetembelea baadhi ya ghala za EHCSS na kujionea mifumo ya kisasa ya uhifadhi na usimamizi wa bidhaa.
Katika kuendeleza ushirikiano huo, taasisi hizo mbili zimekubaliana mambo kadhaa ikiwamo kuandaa makubaliano ya ushirikiano yatakayosaidia kuongeza fursa za bidhaa za Tanzania kuingia katika soko la Misri, kutoa mafunzo ya kitaalam kuhusu usimamizi wa ghala, kubadilishana uzoefu wa matumizi ya teknolojia za kisasa na kuwezesha biashara ndani ya soko la Afrika kupitia Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa na kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

More Stories
FCC,ZFCT zaimarisha ushirikiano
Mha.Mramba akutana na wadau wa Kimataifa kuharakisha miradi ya Jotoardhi
Wakulima wa pamba wafungua akaunti kwa wingi