June 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bajeti 2026/2027 kuchechemua uchumi,uwekezaji


WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Serikali inatarajia kutumia shilingi trilioni 62.3 katika mwaka wa fedha 2026/27, huku sehemu kubwa ya fedha hizo ikitarajiwa kutoka kwenye mapato ya ndani yatakayofikia shilingi trilioni 46.8.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 10,2026 kuelekea uwasilishaji wa Bajeti Kuu ya Serikali utakaofanyika kesho bungeni, Waziri Omar amesema bajeti hiyo itaendelea kuimarisha ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati.


Amesema kabla ya kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2026/27, Serikali itatoa tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/26, ambayo imeonyesha mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani yaliyofikia malengo yaliyowekwa.


Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali itaendelea kuelekeza fedha katika miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), uboreshaji wa mtandao wa barabara, upanuzi wa huduma za maji, miradi ya nishati pamoja na uwekezaji katika maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi.


Akizungumzia maboresho ya kodi, Waziri Omar amesema Serikali imepokea jumla ya mapendekezo 727 kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi, taasisi za elimu, jumuiya za wafanyabiashara na wananchi binafsi kuhusu marekebisho ya kodi, ada na tozo.


Amefafanua kuwa mapendekezo hayo yalifanyiwa uchambuzi na Kamati ya Wataalam wa Maboresho ya Kodi ambapo mapendekezo 125 yalikubaliwa, 295 yakakataliwa, huku mengine yakipelekwa kwa taasisi husika kwa uchambuzi zaidi na utekelezaji.


Aidha, amesema Serikali imepokea ushauri wa ziada kutoka Kamati ya Kiufundi ya ngazi ya juu maarufu kama Think Tank, inayojumuisha wataalam kutoka sekta za umma na binafsi, ili kuhakikisha mapendekezo yatakayowasilishwa bungeni yanazingatia maslahi mapana ya Taifa.


Waziri Omar ameeleza kuwa lengo la maboresho hayo ni kukuza uchumi, kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji, kupanua wigo wa walipa kodi na kupunguza mzigo wa kodi usio wa lazima kwa wananchi na wafanyabiashara.


Amewataka Watanzania kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati, huku Serikali ikiendelea kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha zinatumika kwa ufanisi na tija.