
.
Na Moses Ng’wat, ILEJE.
Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Mkoani Songwe, imetangaza kuimarisha utekelezaji wa sheria na kanuni zinazolenga kuhakikisha wananchi wanajenga na kutumia vyoo bora ili kuboresha afya ya jamii na kudhibiti magonjwa yatokanayo na mazingira duni ya usafi.
Hatua hiyo ilitangazwa Juni 4, 2026 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ileje, Abdala Mayomba, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.
Kikao hicho kiliratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali la EEPCO, ambalo linatekeleza mradi wa kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora katika vijiji 40 kati ya vijiji vya kata 12 kati ya kata 71 za Wilaya ya Ileje.

Mayomba alisema serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa wananchi watakaoshindwa kujenga vyoo bora, ikiwemo kutozwa faini na hatua nyingine za kisheria kwa mujibu wa sheria ndogo za afya na usafi wa mazingira.
Aidha alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Nuru Kindamba, kukamilisha taratibu za matumizi ya sheria ndogo, huku akielekeza watendaji wa kata kuhakikisha ndani ya miezi miwili kaya zote ambazo hazina vyoo bora zinafikiwa na kuhamasishwa kuboresha hali hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya tathmini, Mwakilishi wa EEPCO, Robius Bagoka, alisema kati ya kaya 18,636 zilizofikiwa, asilimia 59.5 zina vyoo bora, asilimia 39.2 zinaendelea kutumia vyoo vya asili, huku kaya 152 sawa na asilimia 0.82 zikiwa hazina vyoo kabisa.

Alibainisha kuwa tatizo pia limeonekana katika taasisi mbalimbali ikiwemo ofisi za vitongoji, vijiji na kata, shule, makanisa, vilabu vya pombe za kienyeji pamoja na maeneo ya mashine za kusaga nafaka ambako baadhi bado hazina vyoo au zinatumia vyoo visivyo bora.
Bagoka alisema wakati mradi unaanza kati ya Oktoba na Desemba 2025, asilimia 51 ya kaya zilikuwa na vyoo bora, asilimia 45 zilikuwa zinatumia vyoo vya asili na asilimia moja hazikuwa na vyoo kabisa, hali inayoonyesha mabadiliko chanya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ileje, Kindamba, alisema awali changamoto ya matumizi ya vyoo bora ilichangiwa na mila na desturi, lakini elimu inayoendelea kutolewa imeongeza mwitikio wa wananchi, akisisitiza lengo si kuwaadhibu bali kulinda afya ya jamii.
Mjumbe wa kikao hicho, Harsoni Chanya, alisema pamoja na hatua za elimu, kuna haja ya kuwepo kwa msaada wa vifaa vya ujenzi wa vyoo bora kwa gharama nafuu kama vile vyoo vya aina ya Sato, sambamba na kuongeza uwajibikaji kupitia utekelezaji wa faini kwa watakaokaidi.


More Stories
CCM yakemea vitendo vya ubakaji,ulawiti,ushoga
Dkt.Nchimbi atembelea Banda la REA
Dkt. Maponga: Watanzania walinde amani dhidi ya ushawishi wa vurugu