Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MJUMBE wa halmashauri kuu CCM taifa (MNEC), Ndele Mwaselela ametaka ujenzi wa uzio katika kituo cha afya Iyela unapaswa kuharakishwa ili kuboresha mazingira ya utoaji huduma na kuongeza usalama kwa wagonjwa pamoja na watumishi wa afya.
Mwaselela amesema hayo wakati akikabidhi matofali 5,000 na mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa uzio huo, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa kata ya Iyela mkoani Mbeya.
Amesema ushirikiano wa viongozi na wananchi utahitajika ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, huku akiwahimiza wakazi wa eneo hilo kushiriki katika shughuli za ujenzi wa msingi na maandalizi mengine muhimu.

“Kituo hiki kinatoa huduma kwa wananchi wa Iyela na maeneo jirani, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha mazingira yake yanakuwa salama na rafiki kwa wagonjwa na watumishi,” amesema Mwaselela.
Kituo cha afya Iyela, kilichojengwa mwaka 2023, kinaendelea kutoa huduma mbalimbali za afya ikiwemo huduma za uzazi, huku wananchi wakieleza kuwa ukosefu wa uzio umekuwa ukisababisha changamoto za usalama na faragha kwa baadhi ya wagonjwa.
Baadhi ya wananchi wa Iyela wameeleza kuwa kukamilika kwa uzio huo kutasaidia kuboresha mazingira ya huduma, hasa kwa wanawake wajawazito na wanaofika kituoni kupata huduma mbalimbali za afya.

Mganga wa kituo hicho, Daktari Godwin Mariatabu, amesema ujenzi wa uzio utaongeza usalama wa vifaa tiba na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa, huku ukiwawezesha wajawazito kufanya mazoezi ndani ya eneo la kituo kwa utulivu zaidi.
Pamoja na hatua hiyo, wananchi wameiomba serikali na wadau mbalimbali kuendelea kuboresha miundombinu mingine katika kituo hicho, ikiwemo ujenzi wa njia za kutembea zilizofunikwa kati ya majengo ili kurahisisha utoaji wa huduma wakati wa mvua.

More Stories
Wanahabari wahimizwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi
REA yaandika historia Ludewa
TMA yatoa utabiri wake msimu wa Juni hadi Agosti 2026