📌Yawasha umeme ukanda wa Nyasa kitongoji cha Nkanda
📌Yapongezwa kufikisha umeme kwenye mazingira magumu Njombe
📌Bodi ya REA yasisitiza wananchi kuchangamkia fursa uwepo wa nishati ya umeme
Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijni (REA), unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali pamoja na kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wote waliopewa na watakaopewa zabuni ya kutekeleza miradi ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa ili iweze kuwanufaisha wananchi.
Hayo yamebainishwa leo Mei 25, 2026 na Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), wakati wa hafla ya kukagua miradi, kutembelea na kuwasha umeme kitongoji cha Nkanda kilichopo wilaya ya Ludewa mkoani Njombe mradi uliokuwa unatekelezwa na Suma Jkt Electric Company Ltd.
Mha. Ahmed Chinemba amesema kuwa, mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji vya mwambao wilayani Ludewa unatekelezwa na mkandarasi M/S SUMAJKT ELECTRIC COMPANY LTD kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 3.2 ili wananchi wa mwambao wapate huduma ya umeme.
“Mradi huu umelenga kuongeza shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa kitongoji cha nkanda ukiwa na chachu ya kutoa fursa za kibiashara kwa kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, kurahisiha upatikanaji wa huduma za kijamii na uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo kama mashine za kusaga, mashine za kuchana mbao pamoja na mashine za kuchomelea,” Amesema Mha. Chinemba.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Suma JKT Brigedia Jenerali Shija Lupi, ameishukuru REA kwa kuwapatia kazi hiyo ya kufikisha umeme katika maeneo ya mwambao kikiwemo kitongoji hicho cha Nkanda ambapo kazi imekamilika kwa ubora.
“Sisi Suma JKT tumefanisha kufikisha umeme kwenye mazingira magumu kama haya ambayo yalikuwa na changamoto nyingi lakini tumefanikiwa na sasa tunaona matunda yake, ” Amesema Brigedia Jenerali Lupi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mha. Deogratius Nagu amesema katika kitongoji cha Nkanda takribani shilingi milioni 450 zimetolewa na Serikali kupitia REA ili kufikisha huduma ya umeme katika kitongoji hicho.

Aidha, amewataka wananchi wa Nkanda kuchangamkia fursa ya uwepo wa umeme kwa kuhakikisha wanafanya wiring katika nyumba zao na kuunganisha umeme kwa wingi ili wanufaike na umeme huo katika kitongoji chao.
Naye, Mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo hilo Bw. Stanslaus Gowele amesema ujio wa umeme maeneo ya mwambao yanakwenda kuongeza chachu ya Maendeleo kiuchumi na kijamii kwa wananchi hao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanufaika wa mradi huo wameeleza namna ambavyo Mradi huo umekuwa mkombozi kwao.


More Stories
TMA yatoa utabiri wake msimu wa Juni hadi Agosti 2026
NIDA yasajili zaidi ya watu mil.1.1 miezi 10
Watuhumiwa kulima bangi zaidi ya ekari 10