May 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kapinga aeleza mpango mpya kuimarisha Viwanda Tanzania

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma


WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judithy Kapinga amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kukuza sekta ya viwanda nchini kwa lengo la kuongeza ajira, uzalishaji na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.


Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo.Mei 22,2026 wakati akiwasilisha taarifa kuhusu maendeleo ya sekta ya viwanda, Waziri Kapinga amesema Serikali inatarajia kuanzisha kongani za viwanda katika wilaya moja kutoka kila mkoa wa Tanzania Bara ili kuchochea shughuli za uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao na malighafi zinazopatikana katika maeneo husika.


Amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za viwanda karibu na wananchi pamoja na kufungua fursa zaidi za uwekezaji na ajira kwa vijana na wanawake nchini.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma za kihandisi kwa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji, matumizi bora ya rasilimali pamoja na kuboresha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.


“Lengo ni kuvifanya viwanda vya ndani kuwa na uwezo mkubwa wa ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa,” alisema Kapinga.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema

Serikali itaendelea kufanya tafiti, kubuni na kuendeleza mitambo, mashine pamoja na teknolojia mbalimbali zitakazosaidia kukuza uzalishaji mali na maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Ameongeza kuwa mkakati huo utaambatana na kuhamasisha utengenezaji wa mitambo hiyo kibiashara ili kuongeza matumizi ya teknolojia za ndani na kupunguza utegemezi wa vifaa kutoka nje ya nchi.


Hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha uchumi wa viwanda na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa.