Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
DIWANI wa Kata ya Buyuni Wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam, Jesca Msolla, amezindua kliniki maalumu ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa lengo la kuwasogezea wananchi huduma muhimu karibu na makazi yao.
Kampeni hiyo ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa iliyoanza Mei 13, 2026, inatarajiwa kuendelea kwa siku 10 hadi Mei 24 mwaka huu katika ofisi ya ktendaji wa Kata ya Buyuni.

Akizungumza kwa niaba ya diwani huyo, Mwenyekiti wa serikali ya mtaa Buyuni, Sylvanus Mwenda, amesema zoezi hilo limeandaliwa na Msolla ikiwa ni sehemu ya kutatua changamoto za wananchi pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Diwani Msolla ameona changamoto kubwa ya wananchi kukosa vyeti vya kuzaliwa, hivyo akaamua kushirikiana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kupeleka huduma hiyo karibu na wananchi ambapo vyeti vinatolewa papo hapo kwa gharama za serikali,” amesema Mwenda.

Mwenda amesema cheti cha kuzaliwa ni nyaraka muhimu inayosaidia wananchi kupata huduma mbalimbali ikiwemo NIDA, hati ya kusafiria, elimu na ajira, huku akieleza kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakikumbana na changamoto kutokana na kukosa vyeti hivyo ambapo pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na RITA kwa kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi.
Kwa upande wake, Mratibu wa kampeni ya kliniki ya RITA wilaya ya Ilala, Heri Shaban, amesema wazo la kupeleka huduma hiyo katika maeneo ya pembezoni limetokana na changamoto waliyoibaini wakati wa zoezi la usajili wa vitambulisho vya Taifa, ambapo wananchi wengi walikosa vyeti vya kuzaliwa vilivyohitajika kupata NIDA.

Amesema hali hiyo iliwalazimu kuwasilisha ombi ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ilala ili RITA ifikishe huduma zake katika kata za pembezoni kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata nyaraka hizo kwa urahisi.
Naye Afisa msajili wa vyeti vya kuzaliwa kutoka RITA, Erasto Wambura, amesema kampeni hiyo inalenga kusaidia Serikali kusogeza huduma karibu na wananchi huku akibainisha kuwa kwa sasa kliniki hizo zimeweka kambi katika maeneo ya Buyuni, Chanika na Gongolamboto.
Serikali kupitia RITA imeendelea kuendesha kampeni mbalimbali za utoaji wa vyeti vya kuzaliwa nchini kwa lengo la kuongeza usajili wa wananchi na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii na kiutawala kama NIDA, elimu, pasipoti na huduma za afya.

More Stories
CRDB Foundation,Zuchu wazindua jukwaa la “Zuchu – IMBEJU Masterclass
Hatifungani ya kwanza yazinduliwa iTrust
Ofisi ya Msajili wa Hazina yafanya mazungumzo na Balozi wa China