June 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kortini kwa kujifanya afisa wa Magereza na kuomba rushwa

Na Israel Mwaisaka, Nkasi 

‎Kijana aliyefahamika kwa jina la Festo  Joseph Mgalima (21) mkazi wa Kijiji Cha Mtowisa Wilaya ya Sumbawanga amefikishwa katika mahakama ya wilaya Nkasi kwa kosa la kujifanya ni mtumishi wa serikali afisa wa jeshi la Magereza na kuomba rushwa ya Tshs,300,000.

‎Akisomewa mashitaka yake na mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo Cedrick Mashauri mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi Adamu Mwanjokolo ni kuwa mnamo Marchi 21,2026 katika Kijiji Cha Mbwendi mtuhumiwa alijifanya ni askari wa jeshi la Magereza na kumkamata mfugaji aliyekuwa akichunga ng’ombe alidai kuwa amechungia mwenye msitu wa Magereza hivyo ametenda kosa.

‎Baada ya hapo mtuhumiwa huyo alianza kuomba rushwa ya fedha ya Tshs.300,000  ili aweze kumuachia  vinginevyo angempeleka  katika gereza la Kitete lililopo wilayani Nkasi kwa kosa hilo la kulisha mifugo kwenye msitu wa Magereza kinyume  cha Sheria

‎Mwendesha mashitaka huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo la kujifanya askari wa jeshi hilo la Magereza wakati siyo na kuwa kosa hilo lipo chini ya kifungu Cha 100 Cha kanuni ya adhabu.

‎Mtuhumiwa alikana shitaka lake na amerudishwa rumande hadi hapo kesi yake itakapotajwa tena Mei 27,2026

‎Wakati huo huo vijana Saba wa Majengo mjini Namanyere wilayani Nkasi wamefikishwa Katika mahakama hiyo kwa kosa la wizi wa kutumia silaha kinyume na kifungu Cha 287 E ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023

‎Watuhumiwa hao mnamo February 22,2026 walimvamia na kumtishia kwa kisu  Anaclara Saninga na kufanikiwa kumpora Doti  27 za vitenge na vipande 30 vya nguo za kike  zote vyenye thamani ya Tshs.706,000

‎Washitakiwa hao ni Raymond Mkulu (19),Respis Peter Kasawanga (34),Baraka Peter Kauzeni (19), Emmanuel Joseph (19),Bruno Fredy Mwaipopo (19),Jesse Lufukunya (25) na Joseph Robert Mgala (44).

‎Watuhumiwa baada ya kusomewa shitaka lao walikana na wamerudishwa rumande hadi hapo kesi yao itakapotajwa tena Mei 27,2026 na kesi hiyo kwa mujibu wa Sheria haina dhamana kwa maana ni ya kutumia silaha.