May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta Handeni wafikia asilimia 77

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Menejimenti ya Wizara ya Nishati imepongeza kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) baada ya ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta cha Sindeni wilayani Handeni kufikia asilimia 77.

Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 13, 2026 wakati Menejimenti hiyo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu wezeshi katika kituo hicho muhimu kilichopo mkoani Tanga.

Katika ziara hiyo, viongozi hao walijionea hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati wa EACOP unaotoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani nchini Tanzania, huku wakieleza kuridhishwa na ubora pamoja na kasi ya kazi zinazofanywa na mkandarasi na wataalamu wa mradi.

Menejimenti hiyo imeeleza kuwa maendeleo hayo yanaashiria dhamira ya kuhakikisha mradi huo mkubwa wa kimkakati unakamilika kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa nchi na wananchi.