May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafugaji watakiwa kulinda ardhi yao

Na Mwandishi wetu,TimesmajiraOline,Simanjiro

NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya ameitaka jamii ya kifugaji kulinda na kuitunza ardhi yao na kuepuka uuzaji holela wa ardhi.

Ole Millya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Simanjiro ameeleza hayo kwenye maadhimisho ya wiki ya wazazi wilaya ya Simanjiro iliyofanyika leo Mei 13,2026 katika kata ya Ruvu Remit.

Amesema wana Simanjiro wanapaswa kuilinda ardhi yao na kutowaachia madalali wa ardhi ambao huwa wanajinufaisha kwa kuuza.

Aliwasihi jamii ya wafugaji kutambua  kuwa ardhi yao ndiyo kimbilio lao katika kulisha mifugo hivyo wasicheze nayo zaidi ya kuitunza.

“Katika maisha yangu nitapambania ardhi ya wafugaji wa Simanjiro mniunge mkono na tumuunge mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani anatupenda wafugaji,” amesema Ole Millya.

“Tatizo la kutafsiri mipaka ya ardhi ya Simanjiro na Kilindi kupitia mikoa ya Manyara na Tanga nimeifikisha kwa Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba na ameahidi kutuma timu ya uchunguzi,” amesema Ole Millya.

Aidha ameeleza kuwa walanguzi wa ardhi wanatumia tafsiri ya mipaka isiyo sahihi kuuza ardhini ila timu hiyo ya Waziri Mkuu itafika na kutafsiri mipaka ipasavyo.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro ,Warda Maulid amesema jamii ya wafugaji inapaswa kupendana na kuachana na migogoro ya ardhi.

“Nawapa salamu za Mkuu wa Wilaya  yetu Fakii Lulandana kuwa tujikite kwenye shughuli za maendeleo na siyo kujihusisha na migogoro ya ardhi,” amesema Warda.

Katibu wa jumuiya ya wazazi wa CCM wilaya ya Simanjiro, Mirumbe Sasi amesema katika maadhimisho hayo wamegawa taulo za kike kwa wanafunzi wasichana wa shule ya sekondari Ngage na kupanda miti 50.

Diwani wa kata ya Ruvu Remit Yohana Maitei (Kadogoo) ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwani hana miradi kiporo iliyobaki katika Kata hiyo.

Kadogoo amesema miradi yote imekamilika na hivi karibuni Ole Millya aliwapatia mil.2 za ununuzi wa madawati katika shule ya sekondari.

“Tuna changamoto ya daraja la mpaka wa Simanjiro na Same mkoani Manyara, tulitoa kiwanja ili kituo cha afya kijengwe ila ni kimya hadi sasa na bwawa la Relumo la Kapoko limekatika na mafuriko yanaathiri Ruvu,” amesema.