May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maisha ya machozi yageuka matumaini

*Vaileth Kimbe atambua mchango wa CAMFED kumuinua kiuchumi

Na Mwandishi wetu

VAILETH Kimbe (30), mkazi wa Kata ya Mwangata mtaa wa Ngelewaya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, hawezi kuzuia machozi anaposimulia historia ya maisha yake.

Safari yake ya kutoka kwenye vilio na maisha magumu hadi kuwa mfugaji wa kisasa wa kuku, imewezekana kupitia msaada wa Shirika la CAMFED.

Utoto wa maumivu na wajibu mzito

Akizungumza na mwandishi wa makala hii,simulizi ya Kimbe ,inaanza kwa kusema,”Kipindi nasoma, mama yangu alikuwa anapitia changamoto kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo mpaka kufikia hatua ya kupoteza fahamu,kwa sababu nilikuwa mdogo nikawa sielewi,”.

Kimbe ni mtoto wa pili katika familia ya watoto wawili kwa mama yake, Ferister Nyalusi,pia ni mtoto wa 11 kwa baba yake, Fidelis Kimbe,anasimulia kuwa mama yake alianza kuugua alipokuwa na miezi mitatu tu.

“Mama aliniweka kitandani na kuanza kupiga kelele. Tangu hapo akapata tatizo la afya ya akili katika makuzi yangu sikubahatika kunyonya maziwa ya mama kutokana na hali hiyo iliyomsumbua kwa muda mrefu,” anasema Kimbe kwa uchungu.

Kimbe anaendele kusimulia,kuwa hali ya mama yake iliendelea kumtesa kwani akisikia kitu cha kushtukiza alikuwa anapoteza fahamu,”Afya ya akili inaweza kupotea kwa muda lakini baada ya miezi sita inarudi tena. Hali hii huwa inaniumiza sana,”.

Maumivu ya kisaikolojia

Kuishi na mama mwenye changamoto hiyo kulimwathiri Kimbe kisaikolojia hivyo kuwa mpweke wakati anakua na kujitambua hali ambayo ilimuumiza.

Kumbukumbu tukio lililomchoma moyoni

“Niliporudi toka shule, mjomba wangu aliniambi kuwa leo mama yako alidondoka kwani mvua ilikuwa imenyesha sana lakini tulimsaidia yupo sawa.Nikiwa kidato cha nne mama yangu aliungua miguu yote miwili wakati akipika bagia,” anasema Kimbe huku akilia na kuongeza:

“Jamii ilimtambua mama yangu,inaweza ikapita hata mwaka mzima lakini hali ikaja kumshitukiza hata akiwa sokoni au kanisani. Nilikulia kwa mama na msaada wa watu tofauti tofauti na Mungu alinisaidia nikafaulu,”.

Elimu na biashara ya kujitegemea

Baada ya kufaulu Kimbe alijiunga na shule ya sekondari iliyokuwa jirani na nyumbani ili aweze kumsaidia mama yake.

“Nakumbuka nilivyofaulu kwenda kidato cha kwanza,mama yangu alisema bora nimefaulu shule za kata maana kwa hali yangu hii,kwani kila sehemu nilikuwa nazunguka na mama,nilikuwa kama mlinzi,” anasimulia Kimbe.

Akiwa kidato cha kwanza, alianza kuuza maandazi na bagia. “Nililazimika kujituma kufanya biashara toka nikiwa mdogo. Mama akiwa katika hali ya ujauzito aliishi maisha ya juu sana, baba alikuwa mtu mwenye fedha. Lakini baada ya kuzaliwa hakuwa na msaada tena,”.

CAMFED yamwokoa na kumuinua

Mabadiliko yalianza akiwa kidato cha pili shule ya sekondari Luhota,anasimulia kuwa “Walikuja CAMFED tukiwa wasichana sita kutoka hapo tukaanza kusomeshwa na shirika hilo. Lakini sikuacha biashara ya kupika bagia ili kuweza kumsaidia mahitaji mama yangu,”.

Hata hivyo anasema kuwa shirika la CAMFED,lilimnunulia daftari, sare za shule na kumpatia fedha za matumizi,ingawa hali bado haikuwa nzuri licha ya msaada huo ambao ulikuwa mkubwa.

Kutoka mkopo wa mil.2 hadi mil.60

Kimbe anasema,baaada ya kumaliza shule, hakukata tamaa,mwaka 2021 shirika la CAMFED lilimkopesha kiasi cha sh. milioni. 2 bila riba kwa ajili ya ufugaji wa kuku wa mayai aina ya sasso. “Nilimaliza mkopo huo mwaka uliofuata na kuomba mwingine wa milioni 2,”.

Mwaka 2025, aliomba mkopo wa tatu wa sh. milioni 5. “Niliingiza kuku 700, lakini walikuja kufa na kubaki 628. Walianza kutaga na nikamaliza mkopo wa awali,”.

Ndoto yake kubwa ilitimia Desemba 2025 alipopokea milioni 26 kutoka CAMFED kwa ajili ya ujenzi wa banda la kisasa la kuku. Awamu ya pili aliingiziwa milioni 34 kwa ajili ya vifaranga,dawa na chanjo hivyo thamani ya mradi wote ni sh. milioni 60.

“Mkopo huu nitarejesha kwa muda wa miaka miwili na nusu. Hauna riba, tunaita riba jamii’,”anaeleza Kimbe.

Matarajio ya kuwainua wasichana wengine

Sasa Kimbe anafuga kuku 628 wanaompa wastani wa trei 17 za mayai kwa siku, sawa na mayai takribani 510. Banda lake jipya lina uwezo wa kuchukua kuku 3,000. “Nimepata ‘sapoti’ ya kuku 1,500 pamoja na ujenzi wa banda kutoka CAMFED,”.

Lengo lake ni kurudisha fadhila kwa jamii

“Kwa kuku 600 nilionao ‘nimeshasapoti’ wasichana 1,500.Nikiwa na kuku 3,000 nataka kusapoti wasichana 3,000 zaidi. Baada ya miezi mitatu sehemu ya mapato nitaitumia kuwezesha wasichana wa vijijini,” anaeleza Vaileth na kuongeza:

“CAMFED ‘inasapoti’ wasichana kwa asilimia 100, lakini bado kuna wengine hawajafikiwa. Nitatoa vitu muhimu, elimu ya kujitambua na mafunzo ya ufugaji.Katika kampuni yangu ya VIO FARM, nitawachukua wasichana kutoka vijijini na kuwawezesha elimu ya ufugaji na mtaji wa laki tano kwa waliohitimu mafunzo,”.

Nini ndoto yake kwa sasa

“Shirika la CAMFED ni mama kwangu,kitu ninachoomba ni kunijengea kituo kwa ajili ya mafunzo ya wasichana waliopo vijijini ambao hawana sehemu ya kusemea,”anasema Kimbe.

Changamoto na msaada wa kitaalumu

Kimbe anaeleza kuwa ufugaji una changamoto hasa magonjwa.”Si kila mtu anatakiwa aingie kwenye mabanda,kuna watu wakiingia kuku wanaacha kutaga mayai kwa asili, kuku wanapata mawazo na kuacha utagaji ndo maana wafugaji wengi hawaruhusu watu kuingia ovyo,”.

Kwa sasa anafanya kazi na wasaidizi, na ameweka kamera kwenye mabanda kwa usalama huku kuhusu soko anasema,”Nina wateja wengi eneo la Ngelewaya, Zizi, mpaka kwa Sengo.wote wanategemea hapa. Kuna mtu alikuwa anafuga lakini ameacha kutokana na usimamizi mbovu,”.

Naye Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Iringa, Daudi Chilagane, amethibitisha kuwa ofisi yake imekuwa ikimpa Vaileth elimu ya kitaalamu ya ufugaji.

“Tumekuwa tukimshauri atengeneze chakula chake mwenyewe badala ya kununua, na kuwa na mashine yake binafsi ili aweze kupata chakula chenye ubora zaidi na kuepuka gharama.Tunawaunganisha na fursa mbalimbali za kiserikali, wakiwemo vijana saba kutoka shirika la CAMFED,”anasema Chilagane.

Mama yake anena

Ferister Nyalusi, mama mzazi wa Vaileth Kimbe, mkazi wa Kijiji cha Kilambo, Kata ya Luhota, Wilaya ya Iringa Vijijini, amefunguka kwa hisia kuhusu safari ya maumivu ya kiafya na furaha ya kuona binti yake akifanikiwa kupitia msaada wa shirika la CAMFED.

Mwanzo wa changamoto: Miezi mitatu baada ya kujifungua

Nyalusi,anasimulia kisa kilichobadili maisha yake, kwa kusema kuwa alimzaa Vaileth Julai 21, 1994. “Baada ya kujifungua nilikaa ndani miezi mitatu bila kumtoa mtoto wangu nje. Lakini alipotimiza miezi mitatu, siku moja nilitoka nyumbani kwenda dukani kumfuata mtu aniliyekuwa namdai fedha zangu,”.

“Baada ya kutoka dukani nilishtuka nikiwa nimelala chini na nimefungwa kamba miguuni na mikononi. Nikaulizwa kinauma nini nikasema mikono na miguu kutokana na kamba nilizofungwa toka hapo nikawa mtu wa kuumwa,”.

Kuishi na ugonjwa na kulelewa na jamii

Nyalusi anasema,licha ya changamoto ya afya ya akili,alijitahidi kuendelea na maisha. “Nikiwa naendelea kupika maandazi (kalimati) na bagia, huku nikiendelea na jitihada zangu, walikuja shuleni kwa Vaileth alipokuwa anasoma na wakachagua wasichana waliopo mbele kitaaluma ili waweze kuwasaidia,” anasema.

Baada ya Vaileth kufaulu, wasiwasi mkubwa kama mama ulikuwa namna ya kumwezesha kuendelea na masomo. “Nilikuwa nawaza atamsomesha vipi.Mungu mwema shirika la CAMFED likamsaidia mahitaji yote ya msingi na fedha za matumizi mpaka kumaliza kidato cha nne,”.

Namna anavyojivunia mafanikio ya mtoto wake

“Mwanangu Vaileth amekuwa mama kwangu, Kufanikiwa kwake ni neema,akiuza mayai na mimi anampa fedha ya matumizi, kusaidia mbolea za shamba na mahitaji muhimu,” anasema kwa furaha.

Shukrani na ombi kwa CAMFED

“Nashukuru shirika hilo kwa kumshika mkono mtoto wangu Vaileth toka alipoanza kusoma mpaka sasa amekuwa mfugaji mkubwa wa kuku,ambalo walimpatia kuku 1,500.Naomba CAMFED wamuogezea kuku wengine 3,000 ili aweze kuendelea kusaidia mabinti wengine wenye changamoto za kimaisha,”anasema Nyalusi.