


Na Mwandisi wetu – Masvingo Zimbabwe
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Kaspar Mmuya ,amewasili nchini Zimbabwe kushiriki Mkutano wa Sita wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri Wanaohusika na Usimamizi wa Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Profesa Palamagamba Kabudi unaofanyika Masvingo, Zimbabwe kuanzia Mei 11 hadi 14,2026.
Mara baada ya kuwasili, Mmuya amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Balozi Suzan Kaganda na kuipongeza Tanzania kushiriki katika mkutano huo unaolenga kujadili maendeleo yaliyopatikana katika utekelezaji wa programu za kikanda na masuala ya kimkakati katika utekelezaji wa afua mbalimbali katika Usimamizi wa maafa kwa nchi za SADC.
Masuala mengine yaliyoelezwa na Mheshimiwa Balozi Suzani ni pamoja na Tanzania kuendelea kuzitangaza fursa zilizopo ikiwemo sekta ya utalii, uchukuzi pamoja na kilimo huku akiahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Zimbabwe.
Sambamba na hayo, mkutano huo utahudhuriwa na wadau mbalimbali wa masuala ya Usimamizi wa Maafa kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo ni fursa kwa Tanzania kuendelea kujitangaza Kimataifa kwa kuwa na mifumo thabiti ya Usimamizi wa Maafa pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya Menejimenti ya maafa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoshiriki katika Mkutano huo wa siku Nne ambapo umekutanisha wadau wa masuala ya maafa kutoka nchi kumi na sita wakiwemo wataalamu kutoka katika ngazi za Kimataifa pamoja na Mashirika ya Umoja wa Kimataifa.

More Stories
Aga Khan Hospital yaja na suluhisho ya changamoto ya Uzito uliopitiliza
Ruth Zaipuna kuipeleka NMB Jukwaa la Kimataifa Cambridge
TPDC yaongoza uchimbaji wa Gesi Songo Songo