May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kishindo cha Pande Marathon,zaidi ya washiriki 2000 kujisajili

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

MBIO zinazofanyika ndani ya Pori la Akiba la Pande (Pande Marathon), msimu wa pili, zinatarajiwa kufanyika Agosti Mosi mwaka huu na zinakuja kivingine.

Mbio hizo zinazoandaliwa na Taasisi ya Kukuza Michezo ya Msakuzi Sports Promotion, msimu huu wa pili zitakuwa za aina yake kwani zinatarajia kushirikisha watu zaidi ya 2,000 kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Tayari usajili wa washiriki wa mbio hizo,unaendelea kwa kasi na unaweza kuvunja rekodi ya msimu uliopita.

Akizungumza baada ya kikao cha Kamati ya Maandalizi ya Mbio hizo juzi, Mwenyekiti wa Msakuzi Sports Promotion Dk. John Kisimbi, aliishukuru Mamlaka ya Usimamizi ya Wanyama Pori Tanzania (TAWA) kuridhia Pande Marathon iendelee kufanyika ndani ya hifadhi hiyo kama sehemu ya kukuza utalii wa Pande

Amesema msimu wa pili wa mbio hizo utakuwa wa aina yake kwani mambo mengi yameboreshwa hivyo wananchi wasipange kukosa.

“Pande Marathon za aina yake na za kipekee sana, washiriki watakimbia huku wakifurahia vifutio vya utalii wa wanyama wa aina mbalimbali na uoto wa asili ambao huongeza mvuto na hamasa kwa wakimbiaji. Hii usipange kukosa kwani ni mtoko wa aina yake,” amesema Dk. Kisimbi.

Tofauti na mbio zingine, Dk. Kisimbi amesema washiriki mbali ya kukimbia na kujenga afya, pili wanafanya utalii na tatu washindi wataibuka na zawadi nono.

Kwa mujibu Dk. Kisimbi Februali 14 mwaka huu ambayo ni ‘Siku ya Wapendanao’, walizindua rasmi msimu wa pili wa mbio hizo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Forest Park Kamsuti, uliopo Mbezi Msakuzi, jijini Dar es Salaam.

“Msimu wa kwanza mwaka jana, tulifanikiwa sana, washiriki zaidi ya 500 walijitokeza na baada ya mbio walipata burudani mbalimbali kama vile live bendi, nyama choma za pori, walipata fursa ya kuangalia wanyama na hakuna aliyetaka kuondoka, safari hii mambo ni moto zaidi.

Kwa upande wake, Mratibu wa mbio hizo, Filbert Mosha amesema siku ya Marathon Agosti Mosi, kutakuwa na burudani ya bendi maalum ya muziki, vinywaji, nyama choma na burudani na huduma nyingine kibao.

“Tutakuwa na mgeni rasmi ambaye tutamtangaza baadaye. Lakini pia siku hiyo tutapata mrejesho na ushuhuda wa msimu uliopita, kutakuwa na surprise nyingi, bendi itakuwa live mara baada ya mbio na washindi kupewa zawadi zao, kwa kifupi tutakuwa na Marathon ya kishindo ambacho hakijapata kutokea nchini,” amesisitiza Mosha.

Amesema usajili unafanyika kidigitali kupitia tovuti www.pandemarathon.store.tz.